Uongozi Ubungo Plaza wazungumzia kutimuliwa Blue Pearl

Muktasari:

Mahakama Novemba 3,2017 ilitoa uamuzi na kuamuru Blue Pearl kulipa deni la Sh5.7 bilioni.

Dar es Salaam. Uongozi wa Ubungo Plaza Limited umesema mpangaji wake, hoteli ya Blue Pearl alikoma kulipa kodi ya pango tangu Mei, 2014.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 9,2017, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ubungo Plaza, Harun Mgude amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kushinda kesi Mahakama ya Ardhi.

"Blue Pearl amekuwa mpangaji wetu tangu mwaka 2006 na mkataba wake ulikuwa wa miaka 15 ambao ungeisha 2021. Alikuwa akilipa vizuri lakini tangu Mei 2014 aliacha kulipa," amesema Mgude.

Amesema kutokana hilo walikwenda kufungua kesi Mahakama ya Ardhi na Blue Pearl wameshindwa, hivyo kutakiwa kulipa au kutoka ndani ya jengo.

"Kama mnakumbuka tuliwahi kumtoa na akarudi kwa amri ya Mahakama ili kupisha kesi kuendelea, lakini Novemba 3,2017 kesi iliisha na ameshindwa na kutakiwa kulipa deni la Sh5.7 bilioni," amesema.

Amesema uongozi wa Blue Pearl umeomba kufanya kikao Jumatatu Novemba 13,2017 ili kujadili jinsi ya kulipa deni hilo.

"Baadhi ya wateja wamehamishiwa hoteli nyingine sijui ni wapi. Ila ieleweke kuwa robo tatu ya mali zilizokuwamo Blue Pearl ni za Ubungo Plaza Limited kama vile fenicha na vitu vingine," amesema Mgude.

Uongozi wa hoteli hiyo ulikuwa ukishughulikia kuwahamisha wateja na haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo.