Indonesia kuwekeza sekta ya kilimo, biashara Mbeya

Muktasari:

  • Wataongeza thamani zao la mpunga na ununuzi

 Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema Serikali ya Indonesia imeonyesha ni ya kushirikiana na uongozi wa mkoa wake kuwekeza katika sekta ya kilimo, biashara na viwanda.

Makalla alidokeza hilo jijini hapa jana baada ya kuzungumza na ujumbe wa nchi hiyo ukiongozwa na Naibu Balozi wa Indonesia nchini, Me Nana na wadau wa sekta ya uwekezaji.

Alisema Serikali ya Indonesia imepanga kushirikiana na Tanzania kuendeleza kilimo na biashara huku ikiweka mikakati zaidi mkoani Mbeya jambo likalosaidia kukuza uchumi.

“Indonesia imeainisha maeneo watakayoshirikiana au kufanya biashara mkoani kwetu kuwa ni kuongeza thamani zao la mpunga, ununuzi na ujengaji wa miundombinu ya soko la ndizi Rungwe, upanuzi wa kilimo cha soya na cocoa inayopatikana Kyela,” alisema Makalla.

Alifafanua kuwa aliuhakikishia ujumbe huo usalama wa kutosha huku akiwataka wananchi kuendelea kuchangamkia fursa zinazojitokeza katika maeneo yao.

Mratibu wa Chama cha Wanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Mkoa wa Mbeya, Emely Malinza alisema wamefurahishwa na sera ya ujumbe huo juu ya kufanya mapinduzi ya uwekezaji kwenye kilimo, biashara na viwanda mkoani hapa.

“Tumevutiwa sana na mtazamo wa hawa wenzetu, kwa mfano walituambia wanataka kufanya kilimo kiwe ni mara tatu kwa mwaka tukitegemea maji ya visima badala ya mara moja kama ilivyo sasa ambapo tunagetemea maji ya mvua,” alisema Malinza.

Alifafanua kuwa ili kutimiza malengo ya nchi hiyo kuwekeza mkoani hapa, alishauri Serikali kufuata na kutekeleza ushauri wao walioutoa ikiwamo kuwekeza kwenye visima vya maji badala ya kutegemea mvua.

Malinza alisema kwamba endapo Serikali ya mkoa itatimiza mambo yote muhimu waliyoshauriwa, TCCIA wataendelea kutoa elimu na kuhamasisha wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda kuchangamkia fursa hiyo.

Mkazi wa Mbeya, Ally Suleiman aliishukuru Serikali kwa jitihada za kutafuta wawekezaji akisema kwamba hiyo ni fursa kwa wananchi wa Mbeya.