JK aenda kuchunguzwa afya Marekani, mkewe apata tuzo

Mke wa Rais, Jakaya Kikwete, Salma, akionyesha Tuzo ya Heshima iliyotolewa na Falme za Kiarabu Dar es Salaam, jana.Picha na Fidelis Felix

Muktasari:

Ameondoka jana atarejea Alhamisi ijayo.

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini kwenda Marekani kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, ilisema kuwa Rais Kikwete aliondoka juzi Jumatano na kwamba kulingana na ratiba ya uchunguzi wa afya yake anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi ya wiki ijayo.

Hata hivyo, taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, haikueleza bayana tatizo linalomsumbua Kikwete mbali ya kusisitiza kuwa amekwenda huko kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.

Taaarifa za hali ya afya ya Rais Kikwete kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 2009, ikiwa ni siku chache tu baada ya kushindwa kukamilisha hotuba aliyokuwa akiitoa kwenye sherehe za miaka 100 ya Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Rais Kikwete alilazimika kukatiza hotuba yake na kwenda kwenye chumba cha mapumziko kwa muda wa dakika 10 kutokana na kile kilichoelezwa na daktari wake kuishiwa nguvu.

Wakati huohuo, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewasili nchini jana akitokea Dubai, Falme za Kiarabu ambako alipata Tuzo ya Dunia ya Hamasa ya Uongozi (Global Leadership Inspiration Award), ambayo msingi wake ni kutambua uongozi madhubuti na hamasa katika kutetea hadhi ya wanawake duniani.

Akizungumza tuzo hiyo alisema: “Tuzo niliyopata ni heshima kubwa kwa wanawake wa Tanzania...hakuna maendeleo ya kweli na endelevu bila wanawake, hivyo lazima jitihada zifanyike kushirikisha wanawake katika sekta mbalimbali za maendeleo.” Mama Kikwete aliwataka wanawake nchini kujitokeza kuzungumzia unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa na wanaume.