JKCI yatoa elimu ya wagonjwa wa moyo

Muktasari:

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni yape nguvu maisha yako 'power your life'.

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) leo imeadhimisha siku ya moyo duniani kwa kutoa elimu kwa wagonjwa wanaohudhuria kliniki kuhusu afya ya moyo.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni yape nguvu maisha yako 'power your life'.

Akitoa mafunzo kwa wagonjwa hao Daktari Bingwa wa Upasuaji na Magonjwa ya Moyo, Peter Kisenge alisema kuna vitu vya kujiepusha ambavyo vinachangia magonjwa ya moyo kama uvutaji sigara, ulaji chakula mbovu, unywaji pombe uliokithiri, kutokufanya mazoezi lakini pia yapo magonjwa yanayosababisha magonjwa ya moyo kama kisukari na shinikizo la damu.

"Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inawaomba wananchi wote Tanzania kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi, ulaji wa vyakula vinavyozingatia afya bora, kutovuta sigara na kuacha kunywa pombe iliyokithiri pia kwa kuwa na taratibu ya kupima afya kuhakikisha magonjwa nyemelezi yanayosababisha madhara kwenye moyo yanatibiwa mapema na vizuri," alisema Dk Kisenge.