JKCI yafanya upasuaji wa kihistoria

Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji kwenye taasisi hiyo, Dk Bashiru Nyangasa (Katikati).

Muktasari:

Upasuaji huo umefanyika kwenye kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyowakutanisha wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya mjini Mumbai nchini India.

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu ndani ya kifua, upande wa kulia na kushoto na kuunganisha kwenye misuli ya moyo ili kuuongezea moyo damu.

 

Upasuaji huo umefanyika kwenye kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyowakutanisha wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya mjini Mumbai nchini India.

 

Akizungumza na vyombo vya habari leo Juni 21 , Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji kwenye taasisi hiyo, Dk Bashiru Nyangasa amesema pamoja na upasuaji huo, jumla ya wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua (open heart surgery) katika kambi maalumu ya siku sita.

 

Amesema wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo, kubadili milango miwili hadi mitatu ya moyo.

 

“Tumefanya upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili. Aidha katika kambi hii kwa mara ya kwanza tumefanya upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu ndani ya kifua upande wa kulia na kushoto na kuunganisha kwenye misuli ya moyo,” amesema Dk Nyangasa.

 

Aidha mtaalamu kutoka Hospitali ya Saifee, Dk Aliasgar Behranwala amesema kambi hiyo iliyoanza Juni 18 hadi 23, inakwenda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa madaktari pamoja na wauguzi.