JKCI yapandikiza mishipa ya miguu kwenye moyo Dar

Muktasari:

Upasuaji huo ulifanywa juzi na jana na madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa India.

Dar es Salaam. Serikali imeokoa zaidi ya Sh200 milioni kwa kufanikisha upasuaji wa kupandikiza mishipa ya miguu kwenye mishipa ya moyo ya wagonjwa wanane iliyoziba.

Upasuaji huo ulifanywa juzi na jana na madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa India.

Kazi hiyo ilifanyika kwa siku tatu kuanzia Jumatatu baada ya ujio wa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai nchini India.

Madaktari hao wamekuja nchini baada ya ahadi ya Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora duniani, Dk Syedna Aliqadr Saiffuddin aliyoitoa kwa Rais John Magufuli ya kuleta madaktari wa moyo alipofanya ziara hapa nchini.

Akizungumza jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa taasisi hiyo, Dk Bashir Nyangasa alisema wamepandikiza mishipa hiyo kwa mafanikio. “Tumeokoa maisha ya Watanzania, pia imetuongezea ujuzi sisi madaktari wa nyumbani. Mishipa hii ya damu ni midogo kama nywele lakini wenzetu wanaifanya kazi haraka na kwa ufanisi,’’ alisema.

Dk Nyangasa alisema madaktari hao walizibua mishipa iliyoziba bila kufanya upasuaji kitaalamu unaofahamika kama catheterization kwa wagonjwa 12. Alisema mishipa ya wagonjwa hao ilikuwa imeziba kwa asilimia 100 na hivyo kusababisha wapumue kwa shida.

Mtalaamu huyo aliongeza kuwa, huduma nyingine zilizotolewa kwa wagonjwa hao ni kutanua milango ya moyo ambayo haikuwa inapitisha damu vizuri na wengine kuwekewa betri za umeme ambazo kitaalamu zinaitwa pacemaker.

Dk Nyangasa alisema tangu mwaka huu uanze, taasisi hiyo na wadau wa nje wamefanya upasuaji wa kufungua na kutofungua vifua kwa wagonjwa 79.

Alisema kama wagonjwa hao wangekwenda kutibiwa India, Serikali ingetumia Sh2.1 bilioni kwa kuwa gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa ni zaidi ya Sh27 milioni.

Dk Yunus Loya wa Hospitali ya Saifee alisema ujumbe wa madaktari kutoka India umefurahishwa na mazingira mazuri ya kikazi ya taasisi hiyo. “Nimetembelea nchi nyingi, lakini hapa nimejionea majengo mazuri na vifaa vya kisasa kuliko nchi zilizoendelea. Hapa watu wanapata huduma ya upasuaji wa moyo bila kujali vipato vyao,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Madhehebu ya Bohora nchini, Zainudin Adamjee alisema kabla ya ujio wa madaktari hao, wengine walikuja nchini na kutoa tiba za macho kwa wakazi 1,535 wa Mkoa wa Arusha.

Alisema mpango wa madaktari kutembeleana kati ya Tanzania na India utakuwa endelevu kama kiongozi wao alivyoahidi.