Rais Magufuli, Edward Lowassa wakutanishwa na Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Muktasari:

Ni baada ya miezi 15 tangu Lowassa alipohamia Chadema wakati CCM ilipompa John Magufuli dhamana ya kupeperusha bendera yake kwenye mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano.

Dar es Salaam. Hatimaye Rais John Magufuli na Edward Lowassa wamekutana kwa mara ya kwanza tangu Uchaguzi Mkuu.

Ni baada ya miezi 15 tangu Lowassa alipohamia Chadema wakati CCM ilipompa John Magufuli dhamana ya kupeperusha bendera yake kwenye mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano.

Lowassa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema chama ambacho kinapinga vikali vitendo vya Rais Magufuli, ambaye ni mwenyekiti wa CCM kiasi cha kutangaza maandamano na mikutano kote nchini kuanzia Septemba Mosi kupinga kile inachokiita ukandamizwaji wa demokrasia na maamuzi ya kutofuata Katiba na sheria.

Ni maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ndiyo yaliyowakutanisha wanasiasa hao wawili waliopambana vikali kwenye mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano Oktoba mwaka jana.

Wawili hao walikutana jana kwenye misa ya shukrani iliyofanyika jana asubuhi kwenye Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam na baadaye hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Rugambwa ulio kando ya kanisa hilo, ambako viongozi wengine wa zamani wa Serikali na dini walihudhuria.