VIDEO-JPM: Serikali haiwezi kukimbilia kuziondoa kaya 1,900 Mwanza

Muktasari:

  • Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wafanyakazi wa uwanja huo mara baada ya kuwasili akitokea Uganda alikohudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aliwataka wananchi hao kutoendeleza makazi yao wakati wakisubiri uamuzi wa Serikali.

 Siku 31 baada ya kutangazwa kwa uamuzi wa kubomolewa nyumba zinazodaiwa kuvamia eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Rais John Magufuli amesema Serikali haiwezi kukimbilia kuziondoa kaya zaidi ya 1,900 na kusema itaangalia njia bora ya kufanya.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wafanyakazi wa uwanja huo mara baada ya kuwasili akitokea Uganda alikohudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aliwataka wananchi hao kutoendeleza makazi yao wakati wakisubiri uamuzi wa Serikali.

Alitoa kauli hiyo baada ya wafanyakazi wa uwanja huo kumweleza changamoto zilizopo zinazosababisha washindwe kuuendeleza kutokana na wananchi kuuvamia licha ya kuwa ulipimwa tangu mwaka 1989 na ramani yake kutolewa mwaka 2003.

Januari 25, furaha ya wakazi wa maeneo ya Kigoto, Mhonze na Kayenze, zote za Manispaa ya Ilelema mkoani humo waliyoipata Oktoba 30 mwaka jana baada ya Rais Magufuli kusitisha ubomoaji wa nyumba zao ilianza kufifia.

Hiyo ilitokana na Serikali kutangaza uamuzi wa kubomolewa kwa nyumba 1,600 za kaya zinazodaiwa kuvamia eneo la uwanja huo huku kaya 664 zinazodaiwa kuvamia eneo la Jeshi la Polisi katika Mtaa wa Kigoto zikiagizwa kusitisha uendelezaji wa maeneo yao kusubiri uamuzi mwingine.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipotembelea na kuzungumza na wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo la Jeshi la Polisi.

Alisema nyumba 1,600 zinazodaiwa kuingilia eneo la uwanja huo inabidi kubomolewa.

Katika mkutano huo, Lukuvi alisema ziara yake ni agizo la Rais Magufuli la kukagua maeneo yanayodaiwa kuvamiwa na wananchi na kumpa taarifa kwa ajili ya uamuzi unaotarajiwa kutolewa ndani ya mwaka huu.

Oktoba 30 mwaka jana, Rais Magufuli alisitisha ubomoaji wa nyumba za wakazi zaidi ya 3,000 wa maeneo ya Kigoto, Mhonze na Kayenze Manispaa ya Ilemela hadi hapo Serikali itakapotangaza uamuzi mwingine, wakati akizungumza na wananchi katikia uzinduzi wa daraja la waenda kwa miguu eneo la Furahisha baada ya kusoma ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye mabango yaliyokuwa yameshikiliwa na wananchi.

Jana akizungumzia suala la wananchi hao alisema, “...Hili suala ni complex kwa sababu wakazi wanaokaa mle ni zaidi ya kaya 1,900. Kaya hizi kuzitoa unazipeleka wapi? Tena bahati nzuri wote walinipigia kura hakuna hata mmoja aliyeninyima kura. Kunipigia wao kura na mheshimiwa pale ndio tuwatoe.

“Lazima tuyaangalie yote kwa pamoja, tutaangalia eneo mnalolihitaji nyinyi la uwanja, kama litakuwa eneo mlilonalo ni kubwa mno tutawapunguzia wananchi nao wakae, ikiwa wamevamia kwenye eneo ambalo uwanja wa ndege wanahitaji nalo tutaliangalia.”

Aliwaomba wananchi wanaoishi katika eneo hilo kutoendeleza maeneo yao mpaka suala hilo litakapomalizika.

“Nilishamtuma waziri na naibu waziri nasubiri ripoti yao. Lakini kiukweli hatuwezi Serikali ya CCM ikafikia hatua kuwafukuza wananchi wenye kaya zaidi ya 1,900. Uwanja ni wetu, wananchi ni wetu, ardhi ni yetu na waziri wa ardhi na naibu waziri tena ni mwana CCM wa hapahapa na hao hao ndio walinipigia kura, ni lazima tuangalie utaratibu ulio mzuri zaidi,” alisema.

Aliongeza, “Wapo ambao watakaokuwa kwenye eneo kabisa la uwanja wa ndege lazima wataondoka lakini wale ambao wako pembeni tutaliangalia. Ni pamoja na eneo la jeshi na maeneo mengine.”

Awali, meneja wa uwanja huo, Ester Mandale alisema mbali na changamoto hiyo, pia ipo ya ndege zinazobeba samaki kuzuiwa kutua katika uwanja huo kutokana na ongezeko la kodi hivyo kuzilazimika kutua nchini Kenya.

Alisema tatizo hilo limesababisha kupungua kwa pato la Taifa na la wananchi kwa ujumla lakini pia samaki wanaotoka Mwanza kulazimika kusafirishwa kwa magari kwenda Nairobi.

Meneja huyo pia alieleza kuwa uwanja huo unakabiliwa na changamoto ya jengo la wasafiri pamoja na uzio.

Alipoulizwa kuhusu gharama za ujenzi wa jengo hilo pamoja na uzio, meneja huyo alisema bado wanafanya tathmini na kwamba ataiwasilisha mara atakapokamilisha.

Rais Magufuli alimwagiza meneja huyo kufanya uchunguzi wa ongezeko la kodi hiyo lakini pia aliahidi kufikisha suala hilo kwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango kuangalia kama ndilo tatizo pekee wapunguze ili ndege hizo zianze kutua Mwanza.

Kuhusu jengo la abiria na uzio, Rais Magufuli alisema atalishughulia kwa kuangalia namna watakavyotafuta fedha ili kujenga uwanja huo uwe na hadhi kama viwanja vingine vya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwaagiza wakazi wa mkoa Mwanza kutumia mvua zinazonyesha kupanda mazao mbalimbali ya chakula ili kukabiliana na tatizo la njaa.

Baada ya kuwasili mkoani Mwanza, Rais Magufuli alielekea nyumbani kwake Chato kwa mapumziko.