Ripoti ya Sukari yabaini viwanda hewa

Muktasari:

Ukweli huo umebainika katika ripoti ya uchunguzi uliofanywa na kamati teule


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati yake teule yamebaini kuwapo viwanda hewa vilivyokuwa vinaagiza sukari ya viwandani.

Amesema Machi 14, mwaka huu amepokea ripoti hiyo yenye idadi ya viwanda 30 huku viwanda vinane tu ndiyo vikibainika kuwa na taarifa za kweli katika uagizaji wa sukari.

Ametaja kampuni zilizoagiza sukari bila kudanganya taarifa zake ni pamoja na kiwanda cha kiwanda cha kutengeneza kinywaji maarufu cha Coka Cola cha Bonite Bottlers, Nyanza Bottling Company Limited (NBCL) na viwanda vya kuzalisha unga wa ngano vya Bakhresa.

Kauli hiyo ameitoa leo Machi 19, 2018 wakati wa mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, uliobeba maudhui ya ‘Tanzania ya Viwanda na Ushiriki wa sekta binafsi nchini.’

“Viwanda vilivyokuwa vinaagiza industrial sugar kihalali ni viwanda nane tu, viwanda vingine 22 vimebainika kuwa na makosa, vinaagiza kuliko mahitaji yake, mfano kuna kiwanda ambacho bado hakijakamilika lakini kimeagiza tano 500,000, kumbe kuna viwanda hewa, nilikuwa najua kuna wafanyakazi hewa tu,”amesema.

 

Amesema mahitaji ya sukari ni tani 590 kwa mwaka, mahitaji ya viwandani nchini ni tani 135 huku inayotumika kwa matumizi mengine ni tani 455.

Katika matokeo ya ripoti hiyo rais ametolea mfano katika uwekezaji wa soko la mafuta nchini, akisema hakuna umuhimu wa kuagiza mafuta nchini ilihali kuna uwezo wa kuzalisha ndani.

“Mahitaji ni tani 150,000 ya mafuta kwa mwaka, uwezo wa kuzalisha ni tani 135,000, mahitaji yanayobakia tunatumia dola kuagiza mafuta hayo nje, ambayo wakati mwingine quality yake ni ya chini, hasara tunayopata ni kupoteza fedha za kigeni ambazo zingefanya kazi nyingine, kupeleka ajira nje na kuua kilimo cha zao hilo,”amesema rais Magufuli.

“Kwanini tangu uhuru tunaagiza nje mafuta? Why tusiwe na uwezo kuzalisha wenyewe hapa ndani?” Amehoji.