JPM aingilia kati tuhuma za mtendaji kubaka mwanafunzi

Rais John Magufuli

Muktasari:

Mtoto huyo anayesoma katika moja ya shule za msingi jijini Mwanza, anadaiwa kubakwa na Mtendaji wa Kata ya Mkuyuni, James Chilagwile katika matukio manne tofauti yaliyotokea Novemba mwaka jana.

Mwanza. Rais John Magufuli ameingilia kati tukio la kubakwa na kulawitiwa kwa mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye miaka 12, kwa kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatilia ili haki itendeke.

Mtoto huyo anayesoma katika moja ya shule za msingi jijini Mwanza, anadaiwa kubakwa na Mtendaji wa Kata ya Mkuyuni, James Chilagwile katika matukio manne tofauti yaliyotokea Novemba mwaka jana.

Akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure, wajumbe wa sekretarieti ya mkoa na waandishi wa habari jana, Mongella (pichani chini) aliusoma ujumbe aliosema umetoka kwa Rais Magufuli ukimuagiza kufuatilia suala hilo baada ya kuwapo madai ya kutaka kuvuruga upelelezi wa tukio hilo.

Katika ujumbe huo, Mongella aliwataja kwa majina baadhi ya watendaji na maofisa wa Serikali na vyombo vya dola (majina tunayahifadhi kwa sasa), wanaodaiwa kula njama za kumnyima haki mwathirika wa tukio hilo kwa nia ya kumlinda mtuhumiwa.

Orodha hiyo inajumuisha maofisa wa polisi kitengo cha upelelezi na dawati la jinsia, mahakimu na maofisa ustawi wa jamii ambao kwa sasa tunahifadhi majina yao kwa sababu hatukuwapata jana kuzungumzia tuhuma hizo dhidi yao.

“RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa), nakuagiza uhakikishe upelelezi wa tukio hili unafanyika kwa weledi. Mganga mfawidhi na wewe uhakikishe mtoto huyo anatibiwa ipasavyo,” aliagiza Mongella.

Mongella suala hilo tayari limefikishwa mahakamani kupitia shauri namba 239/2016, lakini kuna harufu ya kutaka kuvuruga makusudi kesi hiyo kwa nia ya kumlinda mtuhumiwa, ambaye yuko nje kwa dhamana licha ya mtoto aliyebakwa kulazwa hospitalini.

Kwa mara ya kwanza, gazeti hili lilifichua tukio hilo Novemba 17 mwaka jana baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo dhidi ya polisi kufumbia macho suala hilo.

Baada ya taarifa hiyo kuchapishwa gazetini, uongozi wa polisi ambao licha ya tukio hilo kuripotiwa tangu Novemba 14 mwaka jana, ulidai kutolijua na kutishia kuchukua hatua dhidi ya mwandishi kwa madai ya kutoa taarifa bila idhini ya ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC)