JPM amshukia mbunge wa CCM Morogoro

Rais John Magufuli akizungumza na wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu waliosimamisha msafara wake kutaka azungumze nao jana alipokuwa akirejea jijini Dar es Salaam kutoka Dodoma. Picha na Ikulu.

Muktasari:

Magufuli alikuwa akisisitiza wito wake kwa wafanyabiashara walionunua viwanda wakati Serikali ilipoamua kuvibinafsisha, lakini wakaamua kuvitumia kwa shughuli nyingine au kuvitelekeza.

Morogoro. Rais John Magufuli jana alimshukia Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood akimtaka arejeshe viwanda alivyonunua serikalini iwapo hana uwezo wa kuviendesha.

Magufuli alikuwa akisisitiza wito wake kwa wafanyabiashara walionunua viwanda wakati Serikali ilipoamua kuvibinafsisha, lakini wakaamua kuvitumia kwa shughuli nyingine au kuvitelekeza.

Akizungumza na wananchi aliposimama Kituo Kikuu cha Mabasi Msamvu mjini Morogoro, Rais alisema bila ya kujali aliyenunua kiwanda ametoka chama gani, ni lazima warejeshe serikalini iwapo hawawezi kuviendesha.

“Narudia wito wangu niliokwishatoa kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha na leo nataja, akiwemo mbunge wa hapa wa CCM, narudia akiwemo mbunge wa hapa wa CCM alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha, avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu” alisema Rais ambaye alikuwa njiani kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza mapumziko mkoani Geita na kufanya ziara mikoa ya Kagera, Kigoma na Tabora.

Kauli ya Rais Magufuli imekuja wakati viwanda zaidi ya 10 mkoani Morogoro vikiwa vimefungwa kwa sababu tofauti.

Vikiwa na teknolojia ya zamani, viwanda vingi vimeshindwa kukabiliana na ushindani dhidi ya bidhaa kutoka nje ambazo zinazalishwa kwa gharama nafuu na hivyo kuwa bei rahisi.

Mazingira hayo na mengine kama ya kukosa soko, yamevifanya viwanda vingi kujiendesha kwa hasara.

Aliyekuwa ofisa utawala wa kiwanda cha Magunia (TPM 1998 Ltd), Norender Kumar alisema walilazimika kukifunga kutokana na soko la ndani kuyumba kwa kuwa walikuwa wakiuza asilimia kubwa ya magunia kwa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) ambayo baadaye ilisitisha kununua magunia hayo.

Akizungumzia agizo hilo la Rais, Ofisa Biashara Manispaa ya Morogoro, Gerhard Haule alisema maelekezo ya Rais yalishaanza kufanyiwa kazi na kwamba kiwanda cha mafuta ya kula cha Moproco kinachomilikiwa na mbunge huyo kinatarajiwa kuanza kazi mwezi ujao.

“Tulitembelea kiwanda hiki na tulikuta tayari malighafi zilishaletwa na alituahidi kwamba kitaaanza uzalishaji rasmi mwezi ujao,” alisema Haule.

Haule alisema Mbunge huyo ambaye jana hakupatikana kuzungumzia suala hilo, pia aliahidi kufufua kiwanda chake cha sabuni.

Ofisa biashara huyo alisema Abood pia anamiliki kiwanda cha viatu ambacho pia ameahidi kuanza taratibu za kukifufua.

Hivi karibuni, mbunge huyo alimwambia mwandishi wetu wa Morogoro kuwa ufufuaji wa kiwanda cha Moproco upo katika hatua za mwisho.

Akizungumzia kusuasua kwa uwekezaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Mkoa wa Morogoro, Mwadhini Miyanza alisema wanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo kuboresha nishati, huduma ya maji na miundombinu ya usafirishaji.