JPM amtaka CAG akague kwa kina madini, wabunge wafurahia kamati

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Rais Magufuli aliagiza ukaguzi wa kina wa sekta hiyo jana baada ya kukabidhiwa ripoti ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka jana na mkaguzi huyo.
  • “Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka,” alisema Rais akinukuliwa na taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Rais.

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akague kwa kina sekta ya madini, wabunge wamepokea kwa furaha mpango wa kuunda kamati ya Bunge kuchunguza biashara ya madini nchini.

Rais Magufuli aliagiza ukaguzi wa kina wa sekta hiyo jana baada ya kukabidhiwa ripoti ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka jana na mkaguzi huyo.

“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka. Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka,” alisema Rais akinukuliwa na taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Rais.

“Nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili Watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa.”

Rais aliagiza ukaguzi ulenge kubaini mianya yote inayosababisha nchi kukosa mapato makubwa, hususan katika misamaha ya kodi, mikataba na ulipaji wa kodi.

Agizo hilo la Rais limekuja ikiwa ni siku moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahidi kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza wanufaika wa biashara hiyo pamoja na mikataba yote ya madini.

Pia ni siku moja tu baada ya Rais kutengua uteuzi wa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini , Profesa Justin Ntalikwa aliyeongozana na Spika Ndugai wakati alipotembelea bandarini juzi.

Tanzania ni nchi ya nne kwa uchimbaji madini Afrika ikiwa nyuma ya Afrika Kusini, Mali na Ghana. Sekta ya madini ilikuwa ikiendeshwa na Serikali pekee hadi miaka themanini iliporuhusu wachimbaji wadogo. Katika miaka ya tisini, sheria zililegezwa zaidi kuvutia kampuni ambazo zingeweza kuuza nje bidhaa zitokanazo na madini na pia uwekezaji wa kampuni kubwa za nje ambazo zilianza uchimbaji mkubwa.

Mabadiliko hayo makubwa yanaonekana katika Sera ya Madini ya mwaka 1997, Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na ya mwaka 2010, ambayo iliongeza mrabaha na kulazimisha kampuni za uchimbaji kusajiliwa katika Soko la Hisa na kuipa Serikali umiliki katika miradi yote mipya ya uchimbaji madini.

Wabunge wapongeza kamati

Wakizungumzia uamuzi wa Spika Ndugai kuunda kamati, wabunge waliohojiwa na Mwananchi walisema hiyo ni fursa ya kulijadili kwa kina na kupata ukweli kuhusu mchanga huo wa madini.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche alisema ingawa usafirishaji wa mchanga umelisababishia taifa hasara, siku zote makontena yamesafirishwa kihalali na kwa mujibu wa sheria na mikataba ambayo taifa limesaini.

Alisema kulisahihisha hilo hayahitajiki matamko, bali kukusanya taarifa za kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa kama ya Jaji Mark Bomani ambayo ilituma mtu hadi Japan kufuatilia suala hilo, ili zijadiliwe bungeni.

“Sheria zililetwa na kupitishwa kwa hati ya dharura, kuzuia kwa ghafla tu vitu vilivyo kwenye mikataba ni kusababishia nchi hasara kubwa zaidi. Tayari Acacia wametangaza kwamba wanapata hasara ya dola milioni moja za Kimarekani kwa siku baada ya mchanga wao kuzuiwa,” alisema Heche. “Serikali ilete hiyo mikataba na sheria hizo zilizopitishwa kipindi hicho bungeni tuzifanyie marekebisho. Kuendelea kutoa matamko tu kutasababisha hasara kubwa kwa nchi,” alisema.

Naibu katibu mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya alisema kuundwa kwa kamati hiyo kutaleta unafuu na ufumbuzi wa suala hilo kwa sababu matokeo yataletwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.

Alisema ingekuwa kamati ya Serikali, wangekuwa na wasiwasi lakini kwa kuwa ni ya Bunge wanaamini ripoti yake itawasilishwa kwenye chombo hicho cha kisheria.

Sakaya, ambaye alisema amekuwa akihoji suala hilo tangu mwaka 2011, alisema kamati za serikali zina tabia ya kuyeyuka kama ilivyokuwa ya Operesheni Tokomeza.

“Wakati huo Waziri alikuwa William Ngeleja, lakini sikupata jibu la msingi zaidi ya kuambiwa Taifa halina kazi nao kwa sababu hakuna teknolojia ya kuchenjua makinikia hayo,” alisema.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM wa mkoa, alisema ripoti ya kamati hiyo itaibua mjadala mpana wa kulisemea suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Alisema alianza kulilalamikia suala hilo tangu akiwa mwenyekiti wa wilaya na baadaye mkoa , lakini hakuna aliyesikiliza.

“Ninafahamu mengi kuhusu huo mchanga kwa sababu nipo huko miaka mingi. Ninajua nini kinaendelea, lakini nisiende mbali zaidi tusubiri kitakachobainishwa na kamati itakayoundwa,” alisema Msukuma.

Akiunga mkono hoja ya suala hilo, mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema jambo la msingi ni kuangalia zaidi sheria ya madini inasemaje.

“Hapa waziri wa sheria na wa madini wakutane wajadili kwa kina kuhusu mikataba ya hao wasafirishaji na sheria zinasemaje kwa ujumla,” alisema Waitara.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemshauri Rais Magufuli kukutana na kuzungumza na wawekezaji wanaosafirisha mchanga wa madini nje ya nchi ili kuweka mambo sawa na kuepusha hasara zaidi.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeonyesha wasiwasi wa Serikali kushitakiwa katika mahakama za kimataifa kutokana na zuio hilo.

Akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo, mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare alisema matarajio ni kwamba kampuni za madini zitaipeleka nchi katika mahakama ya kimataifa. Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwaondoa hofu na kuwataka kutulia kwa sababu Serikali na mihimili mingine ya nchi, tayari imechukua hatua na wataeleza matokeo baada ya uchunguzi kukamilika.

Ripoti ya CAG

Awali, Profesa Assad alimkabidhi Rais Magufuli ripoti hiyo ambayo imegusa ukaguzi wa hali ya hesabu za Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya Deni la Taifa na usimamizi wa rasilimali watu.

Mengine ni usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme (Tanesco).

CAG alishauri Serikali kufanyia kazi mapungufu yanayojitokeza kama mianya ya upotevu wa fedha za umma hasa katika madini.

Mengine aliyoyaainisha ni kuiepusha Tanesco kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kielektroniki za risiti (EFD).

Kadhalika, Rais alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na mawaziri wote, makatibu wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na wakuu wa taasisi za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu ya taasisi yake na kuchukua hatua.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati,” alisema Rais.

Majaliwa azuia makontena 180

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefanya ziara Kahama mkoani Shinyanga jana jioni, alizuia makontena 180 yaliyokuwa yamehifadhiwa katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi hadi hapo uchunguzi kuhusu kiwango cha dhahabu kilichomo utakapokamilika.

Majaliwa pia aliamuru kufunguliwa makontena zaidi ya matatu na alichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.