JPM aombwa kutekeleza ahadi ya JK

Rais John Magufuli.

Muktasari:

  • Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kijiji cha Orkeju Loongishu katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Arusha wilayani humo walidai hadi Kikwete anaondoka madarakani mwaka jana hakuwa amekamilisha ahadi yake jambo linalowapa machungu wafugaji hao.

Longido.Wananchi wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha wamemwomba Rais John Magufuli kukamilisha ahadi aliyoitoa mtangulizi wake Rais mstaafu Jakaya Kikwete ya kuwapa ng’ombe wa kifuta machozi  baada ya idadi kubwa ya
mifugo kufa kutokana na ukame ulioathiri wilaya hiyo mwaka 2009.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kijiji cha Orkeju Loongishu katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Arusha wilayani humo walidai hadi Kikwete anaondoka madarakani mwaka jana hakuwa amekamilisha ahadi yake jambo linalowapa machungu wafugaji hao.
Mkazi wa kijiji hicho, Michael Laizer alisema mwaka 2011 walipokea ng’ombe zaidi ya 5,700 wakati walitakiwa kupokea  ng’ombe 11,280 hivyo kumwomba Rais Magufuli akamilishe ya mtangulizi wake ambaye alikua kiongozi mkuu  wa nchi na wananchi wana imani kuwa itatetekelezwa kutokana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema wakati ule Kikwete aliweza kutoa sehemu ya ng’ombe zaidi ya 5,700 kwa sababu safu ya viongozi kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa ilikua ya chama tawala lakini itakua vigumu kwa uamuzi walioufanya katika uchaguzi uliopita kumchagua mbunge ambaye hana mawasiliano ya moja kwa
moja na Rais Magufuli.