JPM asisitiza hatotoa chakula

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli amesema kuna watu walidhani atawapelekea chakula lakini amesema hatofanya hivyo huku akisisitiza asiyefanya kazi na asile na kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi na afanye kazi.

Kigoma. Rais John Magufuli amesema Serikali yake haiwezi kutoa chakula kwa wananchi ambao wana uhaba wa chakula na kuwataka kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo yao.

Akizungumza wakati akiwa Wilaya ya Kankonko mkoani Kigoma, Rais Magufuli amesema kuwa jukumu la Serikali ni kuboresha miundombinu ikiwamo barabara na umeme.

“Inawezekana wengine walidhani Rais anawaletea chakula, siwaletei chakula ng’oo! Usipofanya kazi na usile na usipokula ufe. Ni lazima kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi na afanye kazi,” amesema.

Pia amewataka wafanyabiashara hasa katika vituo vya mafuta kulipa kodi.

Magufuli ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Barabara ya kutoka Kabondo hadi Nyakanazi inayogharimu Sh48.75Bilioni kwa bajeti ya Serikali.