JPM atoboa siri ya kushirikiana na China

Muktasari:

Rais Magufuli amesema sababu kubwa ni ile ya kupokea zaidi misaada kutoka Taifa hilo yenye masharti nafuu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amezitaja sababu za Tanzania na nchi zingine za Afrika kuendelea kuukumbatia uhusiano uliopo baina ya nchi hizo na China.

Rais Magufuli amesema sababu kubwa ni ile ya kupokea zaidi misaada kutoka Taifa hilo yenye masharti nafuu.

Pia, amesema sababu nyingine ni uhusiano baina ya China na Tanzania uliojengwa katika misingi ya kuelewana na kuheshimiana.

Rais Magufuli aliyasema hayo katika mkutano wa kidunia uliovikutanisha zaidi ya vyama vya siasa 40 vya Afrika na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) jijini Dar es Salaam jana.

Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika barani Afrika, lakini ni wa pili kidunia baada ya mkutano kama huo uliofanyika Beijing, China, Desemba mwaka jana.

Alisema uhusiano na ushirikiano baina ya Afrika na China ni wa kihistoria na umekuwa ukiongezeka hasa katika nyanja za kibiashara, uwekezaji, kilimo, elimu, sayansi na teknolojia.

“Na hii ndiyo sababu ya misaada ya China kwenye nchi zetu haiambatani na masharti yoyote, hili ndilo hasa nchi za Afrika tunataka, hatuhitaji masharti. Tunahitaji maelewano,” alisema.

Rais Magufuli alisema lazima kuwe na uhusiano ambao pande zote zinanufaika na kuwa sawa na kwamba kinachohitajika kwa sasa ni maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika.

Kiongozi huyo wa CCM alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopo, nchi za Afrika na China zina fursa ya kukuza ushirikiano huo kupitia maeneo mengi kwa kuwa nazo zinahitaji soko la China.

“Kwa idadi ya watu wa China wanaofikia bilioni mbili tukiamua kwenda kuuza majani ya chai au hata pamba yetu, Wachina wangekuja kuangalia mbuga zetu za wanyama tunajua ni kwa namna gani tunaweza kukuza uchumi wetu,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa nchi hizo zinahitaji kuendeleza ushirikiano na China katika ujenzi wa miundombinu, sayansi, teknolojia, utamaduni, fursa za masomo kujenga uwezo wa wananchi, mabadiliko ya tabia nchi na mageuzi kwenye umoja wa mataifa.

“Huu ndio wakati muafaka wa kukuza ushirikiano kati ya Afrika na China,” alisema Rais Magufuli.

Pia, alisema nchi za Afrika zinapaswa kuungana katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kuandaa misingi bora ya kiuchumi na iwapo zitashikamana zitabadili na kukuza uchumi wao.

Kiongozi huyo alieleza kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza dira yake ya maendeleo ya mwaka 2025 inayolenga kufikia uchumi wa kati kwa kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais aliiomba China kuisaidia Tanzania katika ujenzi wa miradi hiyo ikiwamo ujenzi wa kisasa wa reli ya kati, bandari ya Bagamoyo, miradi ya kufufua na kusafirisha umeme na mradi wa makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba ndugu zetu wa China kutuunga mkono katika utekelezaji wa miradi hii mikubwa ya kimaendeleo,” alisema.

Alisema Tanzania imedhamiria kuongoza mapambano ya kiuchumi na ni sahihi kwa mkutano huo kufanyika hapa nchini.

Nchi za Magharibi zapunguza misaada

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha MLPA cha Angola, Adelia Delcavalyo alisema nchi za Magharibi zimepunguza misaada yake kwa Afrika, lakini China imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa nchi hizo.

“Angola tunaamini kuyafikia mafanikio kupitia ushirikiano huu na kwa muda mrefu tumekuwa na ushirikiano wa karibu na China,” alisema.

Alisema kama ilivyo Tanzania, Angola imeandaa mkakati wake wa kufikia uchumi wa kati kwa kuhakikisha wanapambana na umaskini.

Hata hivyo alisema ukongwe wa CCM ndio uliosaidia mkutano huo kufanyika nchini na kwamba unapaswa kutoka na mkakati halisi wa vyama vya siasa katika kukuza uchumi.

“Vyama vipeane uzoefu kwa namna vitakavyoweza kukuza ushirikiano,” alisisitiza.

Haki za binadamu na uchumi

Awali, waziri wa Mambo ya Nje wa CPC, Song Tao alisema ili kufikia misingi ya kiuchumi, nchi za Afrika zinapaswa kuheshimu haki za binadamu.

Tao alisema China iko tayari kuisaidia Afrika katika mipango yake ya kukuza uchumi na kuzishauri nchi hizo zijiandae kulingana na mazingira.

Alivishauri vyama vya siasa vya Afrika kujikita katika kutafuta suluhisho la matatizo ya watu wake hasa katika kupambana na umaskini.

“China imejikita katika misingi ya ujamaa na uchumi wa masoko. China ni imara kutokana na uongozi imara, kwa hiyo ukiwa na uongozi imara utaweza kuleta maendeleo,” alisisitiza.

Wala rushwa wasipewe nafasi

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kimataifa wa CPC, Guo Songiang alivishauri vyama vya siasa kuandaa mkakati kabambe utakaozuia viongozi wala rushwa kuingia madarakani.

Alisema hakuna namna vyama hivyo vitaweza kufikia uchumi wa kati kama viongozi wanaopenda rushwa wataachwa wagombee na kuingia madarakani.

Songiang alisema waliamua kuanzisha kamati za ukaguzi na usimamizi zitakazosaidia kuwabana viongozi wazembe na wala rushwa ambazo zimezaa matunda.

Alisema, hakuna namna nchi za Afrika zinaweza kufikia maendeleo kiuchumi kama suala la kudhibiti rushwa halitawekewa mikakati imara.

“Inawezekana kabisa Afrika kudhibiti rushwa, msiruhusu viongozi wala rushwa. Hawa ni hatari sana kwa maendeleo,” alisema.

Songiang alisema lazima kila nchi iwe na chombo cha kudhibiti rushwa chenye uwezo wa kuidhibiti, kuwakamata, kuchunguza, kuendesha mashtaka na kufilisi mali zote zilizopatikana kwa rushwa.

Mjumbe wa Chama cha MDS cha Chad, Saleh Bachar alisema ushirikiano unaopaswa kuendelezwa kwa nchi za Afrika na China ni lazima uwe wa maendeleo.

Alisema kwa kuwa chama hicho kimejikita katika kuwaondoa watu wake kwenye umaskini, mikakati inayofanywa inapaswa kuwezesha ustawi wa watu.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema CCM inaamini kwamba binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.

“Afrika ilifanikiwa kukata minyororo ya ukoloni, hivyo kazi kubwa ya viongozi wa sasa ni kukata mirija ya unyonyaji ili Afrika iweze kuwa na uchumi imara na unaojitegemea,” alisema.

Wajumbe wa mkutano huo wamejikita kujadili vitendo na nadharia za vyama vya Afrika na CPC katika kufanya uchaguzi na njia sahihi za kujiletea maendeleo zinazoendana na mazingira ya Afrika.