JPM awaonya viongozi wanaobughudhi machinga

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais amesema hayo jana baada ya kutoka katika Hospitali ya Bugando, kumjulia hali dada yake, Monica John Magufuli aliyelazwa kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) hospitalini hapo.

Mwanza. Rais John Magufuli amewapiga marufuku viongozi wa halmashauri kuwanyang’anya bidhaa wafanyabiashara wadogo na badala yake ameagiza viongozi wote nchini kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi ikiwamo ukosefu wa soko la mazao yao.

Rais amesema hayo jana baada ya kutoka katika Hospitali ya Bugando, kumjulia hali dada yake, Monica John Magufuli aliyelazwa kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) hospitalini hapo.

Alitoa agizo hilo baada ya wakazi wa Sengerema kulalamika kwamba halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya wakulima na wafanyabiashara mananasi wanayouza mjini hapo.

Amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.

“Nilishasema viongozi wote niliowateua mimi msisherehekee uteuzi, mtasherehekea siku mkimaliza uongozi, nataka mchape kazi, tatueni kero za wananchi na waleteeni maendeleo” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, akiwa ameambatana na Rais, alisema hajasikia bugudha yoyote wanayopata machinga wilayani Sengerema na akaahidi kufuatilia na kupata suluhu.

“Rais, nitafuatilia suala hili kwa ukaribu na nitahakikisha ninafanikiwa katika kupata majibu yake,” alisema Mongella.

Mmoja kati ya wafanyabiashara hao, Fredy Wedi alisema polisi na maofisa wengine wa usalama wamejenga mfumo wa kuwanyang’anya bidhaa zao bila kufuata taratibu na kisha kuzigawa kwa watu wengine.

“Polisi wanatuvamia, wanakusanya bidhaa zetu na baadaye wanawapelekea wanafunzi hata bila kutupa sababu za msingi,” alisma.

Agosti 11 2016, Rais Magufuli akiwa jijini Mwanza kwenye ziara ya kutoa shukrani kwa watu wa mkoa huu, alitoa maagizo ya Machinga kutohamishwa hadi pale mamalaka husika zitakapowatengea maeneo rafiki katika biashara zao.

Jana, Rais alisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali akiwa ameambatana na abiria waliokuwa wanatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Akiwa njiani kuelekea Chato kwa mapumziko, Dk Magufuli aliwahakikishia wananchi waliokusanyika barabarani kumsalimia kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.

Alisema katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi minane, kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 3,060, kufufuliwa kwa ATCL na ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Pia alisema watoto wanapata elimu bure na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua uwigo wa ajira na kukuza uchumi wa nchi.