JWTZ kukabidhiwa eneo lenye mgogoro wa ardhi

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara, ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Adam Malima

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo alisema: “Kila upande umeendelea kushikilia msimamo wake na hivyo ufumbuzi kushindikana huku mapigano yanayosababisha majeruhi na vifo vya wananchi wasio na hatia yakishuhudiwa kwa miaka kadhaa; Rais Magufuli akiridhia (maombi) tutalichukua kwa matumizi ya jeshi.

Musoma. Baada ya muafaka kuhusu mgogoro wa mpaka unaohusisha vijiji vitatu vya wilaya tatu za mkoa wa Mara kushindikana, eneo hilo sasa litatwaliwa, kubadilishwa matumizi na kukabidhiwa kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo alisema: “Kila upande umeendelea kushikilia msimamo wake na hivyo ufumbuzi kushindikana huku mapigano yanayosababisha majeruhi na vifo vya wananchi wasio na hatia yakishuhudiwa kwa miaka kadhaa; Rais Magufuli akiridhia (maombi) tutalichukua kwa matumizi ya jeshi.

Vijiji vinavyogombania eneo la mpaka linalodaiwa kuwa na rutuba na kufaa kwa uzalishaji kwenye sekta ya kilimo ni Mikomariro wilayani Bunda, Sirorisimba (Butiama) na Remg’orori (Serengeti).

Malima alisema mgogoro huo licha ya kuhatarisha amani na usalama, pia umezorotesha shughuli za maendeleo kutokana na wananchi wa vijiji hivyo kutoweza kutumia eneo lenye mgogoro.

Wakitoa maoni yao kuhusu mpango wa Serikali wa kutwaa eneo la mgogoro, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Sirorisimba, Nyambura Masiaga na Helan Nyamhanga walisema uamuzi huo utamaliza mapigano ya mara kwa mara kati ya wakazi wa vijiji vinavyogombania mipaka. “Eneo linalogombaniwa likichukuliwa na jeshi itakuwa ndiyo mwisho wa mgogoro kwa sababu hakuna kijiji kitakachoonekana kushinda kwenye ugomvi huu; tumeishi kwa hofu ya vita kwa muda mrefu, ni bora iwe hivyo,” alisema Masiaga.