JWTZ watua Mererani, watoa onyo

Muktasari:

  • JWTZ imesema haitarajii kukwamishwa na mtu yeyote na haitakuwa tayari kukwamishwa kwa namna yoyote katika ujenzi wa uzio.

Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli aliyelitaka kujenga uzio kuzunguka kitalu A hadi D katika eneo la madini ya Tanzanite Mererani, wilayani  Simanjiro.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana Jumatano mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.

Meja Jenerali Michael Isamuyo akiwa na wataalamu wa JWTZ wamefika Mererani leo Alhamisi kukagua eneo lenye vitalu vya Tanzanite.

Ukaguzi huo umefanywa wakiwa kwenye helikopta angani na baadaye ardhini kwa kutumia magari na kutembea kwa miguu.

Akizungumza baada ya kutua katika uwanja wa wazi wa Mererani, Meja Jenerali Isamuyo amesema JWTZ imeanza kutekeleza agizo la Rais na Amiri Jeshi Mkuu na ipo tayari kukamilisha kazi kama ilivyokusudiwa.

Taarifa ya Ikulu imesema baada ya kutembea kwa miguu katika eneo la vitalu A hadi D amebaini linalopaswa kujengwa uzio huo ni la kawaida na ametaka wananchi watoe ushirikiano wa kutosha wakati wa ujenzi.

Ameonya kuwa, wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo JWTZ haitarajii kukwamishwa na mtu yeyote na halitakuwa tayari kukwamishwa kwa namna yoyote.

Baadhi ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara waliokuwepo katika ukaguzi huo wamempongeza Rais Magufuli kwa agizo la kujengwa uzio. Wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa ujenzi.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Hamis Kim, maarufu Komandoo na Katibu wa wachimbaji tawi la Mererani, Aboubakar Madiwa wamesema uzio huo utasaidia kuokoa mapato na utoroshaji wa Tanzanite ambao umekuwa ukisababisha Tanzania kupoteza mapato.