KUELEKEA DODOMA: Jaffo aitaka Chemba kupima ardhi

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) Suleiman Jaffo

Muktasari:

Jaffo alitoa agizo hilo jana alipozungumza na watumishi wa wilaya hiyo, alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

Dodoma. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) Suleiman Jaffo ameiagiza Wilaya ya Chemba kupima ardhi kujiandaa na kasi ya ukuaji wa mkoa.

Jaffo alitoa agizo hilo jana alipozungumza na watumishi wa wilaya hiyo, alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

“Ujio wa Serikali mkoani Dodoma unafanya ukuaji wa kasi wa wilaya utakaofanya muwe sawa na mji wa Kibaha (Wilaya iliyopo Mkoa wa Pwani) na hasa barabara hii (kutoka Dodoma hadi Manyara kwa kiwango cha lami)ikikamilika,” alisema Jaffo.

Alisema kujengwa kwa barabara inayokwenda mkoani Manyara, kutaongeza ukaribu wa wilaya hiyo na ile ya mjini Dodoma, hivyo kuchochea maendeleo ya wakazi.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Chemba, Silivatus Mashimba alisema wilaya imejiandaa kushirikiana na wadau kukuza uwekezaji na kuchochea maendeleo.

“Tumejiandaa kushirikiana na wadau ili kukuza uwekezaji na hivyo kuchochea maendeleo ya halmashauri yetu,” alisema.

Mbunge wa jimbo la Chemba, Juma Nkamia alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na tatizo la vitendea kazi hasa magari, hali iliyowalazimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo na katibu tawala kudandia usafiri.