Jafo azibana halmashauri 12 kulipa madeni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo

Muktasari:

  • Jafo amesema hadi Septemba 30 mkopo wa Sh6.6 bilioni ulikuwa umerejeshwa.

Dodoma. Halmashauri 12 ambazo ni wadaiwa sugu wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa zimetakiwa kabla ya Desemba 30 ziwe zimerejesha deni la Sh2 bilioni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ametoa agizo hilo leo Alhamisi.

Halmashauri hizo ni Mwanza, Mbeya, Moshi, Singida, Kigoma, Karatu, Mbinga, Pangani, Mbinga, Morogoro, Igunga na Kongwa.

Jafo amesema hadi Septemba 30 bodi imetoa mikopo yenye thamani ya Sh9.7 bilioni kwa halmashauri 54 nchini.

Amesema hadi Septemba 30 fedha zilizorejeshwa ni Sh6.6 bilioni.

"Halmashauri nyingi zimejitahidi kurejesha mikopo kwa wakati lakini kuna zilizoonyesha usugu katika kurejesha mikopo," amesema.

Amesema kutorejeshwa kwa mikopo kunasababisha halmashauri nyingine kukosa fursa ya kukopa.

Jafo ameiagiza bodi kuangalia utaratibu wa kupitisha mikopo inayolenga ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika halmashauri ili kukuza ajira na uchumi wa viwanda.

"Bodi iache kubweteka, ijipange kimkakati  kujenga uwezo mkubwa wa kutoa mikopo kwa halmashauri zilizo makini katika mapinduzi ya viwanda," amesema.