Jafo aahidi kuzisaidia shule binafsi

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema hayo jana katika mahafali ya 12 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Baobab.

 Serikali imesema iko tayari kuendelea kuzisaidia shule za binafsi ili kuendelea kufanya vizuri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema hayo jana katika mahafali ya 12 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Baobab.

Alisema atahakikisha Serikali inazisaidia na kuziwezesha shule binafsi ili ziendelee kufanya vizuri na kuwa na ubora hivyo kupunguza msongamano kwenye shule za Serikali.

“Nitahakikisha Serikali inaziwezesha shule hizi ili wazazi waweze kupeleka wanafunzi na hatimaye kupunguza msongamano kwenye shule za Serekali,” alisema Jafo.

Alisema wanaotoa huduma za elimu ni pande mbili, hivyo shule binafsi zimesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kusoma.

Waziri Jafo alisema katika ofisi yake ameanzisha dawati maalumu linalopokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa shule binafsi.

Alisema dawati hilo limemwezesha kubaini changamoto zilizopo kwenye shule binafsi.

Awali, mkurugenzi wa shule hiyo, Halfani Swai alisema kumekuwa na ubaguzi kati ya shule za Serikali na binafsi,

Alitoa mfano akisema wanapotoa motisha kwa wafanyakazi waliofanya vizuri wamekuwa wakikatwa kodi tofauti na shule za Serikali.

“Tumekuwa tukiitwa maneno yasiyokuwa na maadili lakini pia kumekuwa na ubaguzi kati ya shule za Serikali na binafsi hasa kwenye kulipa kodi. Tunaomba utusafishe kwa hilo,” alisema Swai.

Rais wa chama cha wamiliki wa shule binafsi, Ester Mahawe aliishukuru Serikali kwa kuwa karibu na shule binafsi.

Alisema yapo mambo waliyoomba Serikali na imekuwa sikivu, hivyo wana imani hata mengine yaliobaki yatafanyiwa kazi.

“Tunaishukuru Serikali kati yale mambo 16 tuliyokuwa tunalalamikia wameweza kutusaidia, ikiwamo kuziondoa baadhi ya kodi lakini yapo mengine ambayo tunatarajia watatuwezesha,” alisema Mahawe.

Mahafali hayo yamewashirikisha wanafunzi 295 wa kidato cha sita wanaosoma mchepuo wa sanaa, biashara na sayansi.