Jafo ataka wakurugenzi kuepuka ugomvi wa kisiasa

Muktasari:

  • “Kumuona Mkurugenzi afadhali uende mbinguni na ukienda utakuwa umekufa.”

Dodoma. Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) Selemani Jafo amewataka wakurugenzi wapya kuepuka kujiingiza katika ugomvi wa kisiasa utakaokuwa chanzo cha kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Amesema hayo leo Agosti 15, 2018 wakati wa hafla ya kuwaapisha wakurugenzi wapya mjini Dodoma.

“Nendeni mkatekeleze ilani ya uchaguzi msijiingize katika ugomvi utakaowafanya kushindwa kutekeleza majukumu yenu ya kila siku," amesema.

Amewataka pia kusimamia miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG) zinajibiwa kwa wakati unaotakiwa.

Naye katibu mkuu Tamisemi, Mussa Iyombe amewataka wakurugenzi wapya kuhakikisha kuwa wanatenga muda wa kuzungumza na watumishi badala ya kuwaachia maofisa utumishi ambao wamekuwa wajeuri

"Mkurugenzi haingii ofisini, anatafutwa na waziri hapatikani, katibu mkuu hapatikani inashangaza.  Wanawaachia maofisa utumishi wawasikilize watumishi, wajeuri kweli kweli wanaharibu sifa zenu. Kumuona mkurugenzi afadhali uende mbinguni na ukienda utakuwa umekufa," amesema.

Pia amewataka kuheshimu viapo vyao kwa sababu wakifanya mizaha watafungwa kwa kuwa wao ndio maofisa masurufu wa wilaya.