Jafo awaonya ma-DC kuweka ndani watu

Muktasari:

  • Wakati Jafo akitoa agizo hilo, juzi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa saa 48 diwani wa Kitunda, Nice Gisunte.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amekemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo kuwaweka watu ndani.

Wakati Jafo akitoa agizo hilo, juzi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa saa 48 diwani wa Kitunda, Nice Gisunte.

Hata hivyo, Jafo amesema tabia hiyo inasababisha wananchi kuichukia Serikali, hivyo ameagiza wakuu wa wilaya kutumia sheria hiyo kama ilivyokusudiwa na siyo kwa kuonea watu.

Jafo alisema hayo jana jijini Dodoma kwenye kikao kazi na wakuu wa wilaya 27 walioteuliwa hivi karibuni kilicholenga kuwapa maelekezo ya kazi.

Aliwataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.

Katika siku za hivi karibuni, wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia ‘sheria ya saa 48’ kutoa adhabu kwa kuwaweka baadhi ya watu mahabusu.

Mamlaka hayo wamepewa kupitia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 na hutakiwa kutumia amri ya kumweka ndani – kwa muda usiozidi saa 48 – mtu au kundi la watu ambao kubaki kwao nje kunaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.

Baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitumia sheria hiyo kama adhabu au hukumu, badala ya malengo yaliyowekwa ya kulinda usalama wa watu wengine.

Katika kikao na wakuu wa wilaya wapya kilichokuwa na mada kuhusu uhusiano na mawasiliano kazini, Jafo aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu.

Aliwataka kutoa ushirikiano kwa wanaotekeleza ilani ya CCM na si vinginevyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo ikiwamo uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu.

“Kasimamieni ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia mfumo wa kielektroniki na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo, pia mkadhibiti madeni kwa kuwa fedha hizo ndizo zinazotegemewa kwa ajili ya maendeleo,” alisema.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mussa Iyombe aliwataka wakuu wa wilaya kuzitendea haki nafasi walizopewa kwa kufanya kazi wakizingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo na hasa wanapomuadhibu mtumishi aliyekosea. “Serikali ina utaratibu, baadhi ya wakuu wa wilaya walikuwa wanatia aibu, kama kuna mtumishi kakosea, tumia mamlaka zinazomuongoza kumshughulikia na si kusimamisha watu kazi hovyo, kutumbua tumbua hovyo,” alisema Iyombe.

Malalamiko Chadema

Chadema katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana imelaani vitendo vya wateule wa Rais kuendelea kukiuka sheria za nchi, ikilalamikia kitendo cha mkuu wa Wilaya ya Ilala kumuweka ndani diwani wa Kitunda.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene ilisema juzi mchana wakiwa kwenye kikao kwa ajili ya kukagua shughuli za maendeleo katika kata hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa saa 48 diwani wa Kitunda, Nice Gisunte.

Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alikiri kumshikilia diwani huyo kwa amri ya mkuu wa wilaya. “Ni kweli tulimshikilia yule diwani na alilala mahabusu jana (juzi) kama amri ya DC (mkuu wa wilaya) ilivyotolewa,” alisema Hamduni.

Mkuu wa Mawasiliano wa Chadema, Makene alidai mkuu wa wilaya aliyekuwa amefuatana na wanachama wa CCM akihutubia kikao kilichohusu uzinduzi wa kisima cha maji, alitoa salamu za CCM na akasema kisima hicho ni matokeo ya utendaji kazi wa chama hicho, hivyo wana-CCM wanapaswa kujivunia.

Makene alisema Diwani Gisunte aliposimama alitoa salamu za Chadema na akawaeleza wananchi kuwa kisima hicho kimeanza kufanya kazi baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 chini ya uongozi wa diwani wa kata hiyo na meya wa Manispaa ya Ilala ambaye ni kutoka Chadema.

Alidai baada ya Gisunte kushangiliwa na wananchi kwa maelezo yake, ndipo mkuu wa wilaya alipoamuru akamatwe na kuwekwa ndani kwa saa 48.

Makene alisema Gisunte aliwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Stakishari kwenye Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga.

Alisema wanasheria wa chama hicho walikwenda kituoni juzi jioni kumpatia msaada wa kisheria.

Chadema imemtaka mkuu huyo wa wilaya kutoa maelekezo mengine ya kutengua amri yake ikisema ni batili ili polisi imwachie diwani huyo.

Nyongeza na Bakari Kiango