Jafo azungumzia ugumu kutambua idadi miili wanaume, wanawake na watoto

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema hadi leo asubuhi Septemba 23, 2018 haijafanyika tathmini ya kina kujua ni wanawake, watoto na wanaume wangapi waliofariki dunia katika ajali ya MV Nyerere

 

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema hadi leo asubuhi Septemba 23, 2018 haijafanyika tathmini ya kina kujua ni wanawake, watoto na wanaume wangapi waliofariki dunia katika ajali ya MV Nyerere.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Azam wakati maandalizi ya mazishi ya baadhi ya miili iliyopatikana yakiendelea katika kijiji cha Bwisya Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.

Amesema jambo hilo halijafanyika kutokana na pilika zilizopo eneo hilo, hivyo si rahisi kuanza kufanya mchanganuo huo.

"Watu wengi wanataka kutambua miili ya wapendwa wao hivyo si rahisi kuwazuia,’’ amesema Jaffo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula amesema Taifa limepoteza nguvu kazi katika ajali hiyo iliyotokea Septemba 20, 2018 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 225.

"Nasikia katika kivuko hicho watoto walikuwa wengi kwa sababu walienda kununua vifaa kwa ajili ya maandalizi ya shule siku ya Jumatatu (kesho)," anasema Angela.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella leo saa tatu asubuhi amesema baadhi ya maiti zilizokuwa zimezama chini ya maji, zimeanza kuibuka na kuelea na tangu alfajiri hadi muda huo, miili zaidi ya minne imeonekana na kuopolewa katika fukwe ya Bwisya.