Jaji Warioba ataka wahitimu kuandaliwa kujitegemea

Muktasari:

Jaji Warioba amesema kuna haja ya elimu kuendana na siasa za nchi kwa wakati huu.

Dar es Salaam. Rais wa jumuiya ya wanafunzi waliosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema elimu inayotolewa sasa imeshindwa kuwaandaa wahitimu kwenda kujitegemea.

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 20,2017 katika siku ya kwanza ya kongamano lililoandaliwa na UDSM na Taasisi ya HakiElimu kujadili Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda, kufikiria upya sera ya elimu ya kujitegemea.

Jaji Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu amesema ili kupata tija ni lazima elimu iendane na siasa ya nchi ya wakati huu.

Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyofanywa na Serikali kwa miaka 56 iliyopita, kuna changamoto kubwa na hasa ya elimu inayotolewa kutokuwaandaa wahitimu kujitegemea kama ilivyokuwa awali.

"Uwiano wa wanafunzi wanaomaliza shule na wanaoendelea na sekondari ni mdogo, wanaomaliza sekondari na kwenda chuo ni mdogo zaidi," amesema Jaji Warioba

Amesema, "Kuna matatizo makubwa ya miundombinu katika shule na vyuo kama vile madarasa na nyumba za walimu. Vitendea kazi na idadi ya walimu katika ngazi zao na masilahi ya walimu bado ni tatizo."

Jaji Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amesema zamani mtu alikuwa akimaliza darasa la nne akijua kusoma, kuandika na kuhesabu lakini sasa kuna wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

"Siku hizi watu wanamaliza lakini hawana la kufanya, lazima tujiulize elimu yetu ni bora kwa mazingira ya baadaye?" amesema Jaji Warioba.

Amesema wamejaribu kulinganisha sasa na zamani ambako elimu ililenga kujitegemea ndiyo maana wameamua kukutana kujadili.

 

Akifungua kongamano hilo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema Serikali itakuwa tayari kupokea maazimio yatakayofikiwa na washiriki wa kongamano hilo.

"Rais wetu John Magufuli amefurahishwa nanyi wasomi kukutana kujadili ikiwamo suala la uchumi wa viwanda naye amesema atakuwa tayari kupokea mapendekezo mtakayoyafikia," amesema Jafo aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kongamano hilo.

Amesema, "Taifa litajengwa na sisi wenyewe, tutumie kongamano hili kujadili kwa kina kwa kuwa tusipojenga msingi mzuri wa elimu yetu katika ushirikiano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tutakuwa wasindikizaji."

Mkurugenzi wa HakiElimu, John Kalage amesema mjadala huo unafanyika kipindi ambacho wadau wengi waliona kuna haja kutokana na elimu inayotolewa kutowaandaa kujitegemea.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, James Mdoe kwa niaba ya waziri Profesa Joyce Ndalichako amesema wazo la kongamano hilo ni zuri kwa kuwa litajibu maswali mengi kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda.