Jaji Mkuu asema majukumu ya TLS si siasa wala uanaharakati

Muktasari:

  • Ameongeza na kusema iwapo TLS, wanataka kushirikiana na mahakama wabaki katika kazi zao.

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesema Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kinafanya kazi za umma na kwamba hakipaswi kujiingiza katika siasa wala uanaharakati.

Jaji Juma ameyasema hayo leo, Aprili 24 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Jaji  Juma, amesema  majukumu ya TLS  ni kuishauri Serikali, Mahakama, Bunge na kuboresha elimu ya sheria na kusisitiza kwamba TLS ni taasisi ya umma na chama huru cha kitaaluma. 

Jaji Ibrahim amesema ukiangalia kazi za TLS, huwezi kuona siasa wala uanaharakati na kwamba TLS wasikubali kuingia katika siasa wala uanahatakati, wakiingia huko wengine hawatatoa ushirikiano. 

Ameongeza na kusema iwapo TLS,  wanataka kushirikiana na mahakama wabaki katika kazi zao, wakitaka kuwa huru wataachwa wawe huru lakini hawatapata ushirikiano kutoka kwetu sababu wengine haturuhusiwi kuingia katika siasa

“Hapa Tanzania huwezi kutenganisha taaluma ya sheria na Uhuru wa Tanganyika,” amesema.

Amesema TLS ilianzishwa 1954 tukiwa chini ya ukoloni wa Uingereza, wakati huo wanasheria wengine walikuwa ni Wazungu na Wahindi.

1960 na 1961 sheria zilizotungwa wakati wa ukoloni zilijadiliwa ni nama gani zifanye kazi, walifanya mabadiliko ambayo yaliwezesha TLS wabaki na ada zao ambapo zamani zilikuwa ni mali ya Serikali.