Jaji Mkuu awataka wanasiasa, viongozi wa Serikali kutoingilia utendaji wa Mahakama

Muktasari:

Awataka kuacha kuinglia mhimili wa mahakama na kuvunja amri zake

Dar es Salaam.  Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewaonya viongozi wa Serikali na wanasiasa kuacha kuingilia mhimili wa Mahakama na kuvunja amri zake.

Jaji Juma ametoa onyo hilo leo Januari 23, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya sheria yatakayofikia kilele, Februari Mosi mwaka huu.

Amesema kwa mujibu wa Katiba ya nchi mamlaka ya utoaji wa haki ni ya mahakama tu, kutoa wito kwa mahakimu kuchukua hatua kwa wale wote wanaokiuka amri za mahakama.

"Nawakumbusha wananchi na viongozi mbalimbali nje ya mahakama kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama tu," amesema Jaji Juma na kuongeza,

"Ninawasihi viongozi wote wa Serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria wabaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na wajiepushe na kingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na mamlaka ya kikatiba ya Mahakama.”

Kuhusu maadhimisho ya wiki ya Sheria, amesema yatafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuzinduliwa Januari 27 na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne,  Jakaya Kikwete.

Amesema siku ya kilele cha maadhimisho ya wiki hiyo, mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.