Jaji Mshibe awashukia polisi kupika ushahidi, masheha

Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakar

Muktasari:

  • Washiriki wa mafunzo wataka elimu kila mara ili kuhakikisha unakuwapo utekelezaji sheria

Pemba. Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakar amewataka polisi kuachana na tabia ya kuwapikia ushahidi watuhumiwa wa makosa mbalimbali, kwa kuwa kufanya hivyo kunasababisha majaji na mahakimu kutoa hukumu za uongo.

Jaji Mshibe alisema kuna polisi wanaofanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa, makundi ya watu na kwamba hutunga ushahidi ili watu watiwe hatiani.

Alieleza hayo uwanja wa Gombani Chakechake alipokuwa akielezea mambo ya msingi juu ya ukamilishaji kesi kwenye mkutano wa walimu, maofisa ustawi, Polisi, masheha na wanajamii juu ya elimua sheria zinazogusa haki za watoto.

Alieleza kuwa haina maana kila anayefikishwa kituo cha polisi kwa tuhuma tayari ni mkosaji, au wakati mwingine kumtia hatiani kwa tamko la mtu mmoja, kwani kufanya hivyo ni kuendeleza makosa na visasi visivyokwisha ndani ya jamii.

Jaji Mshibe alisema baadhi ya masheha wamekuwa wakikosa ushirikiano na jamii, kwa kuegemea na vyama vya siasa huku wakijisahau wao ni watoa huduma.

Katika hatua nyingine, Jaji Mshibe alisema hivi sasa sheria mpya ya ushahidi namba 9 ya mwaka 2016, ushahidi wowote wa mtoto unakubalika.

Akiwasilisha mada ya haki na wajibu wa mtoto katika sheria ya elimu ya mwaka 1982 na sheria ya mtoto namba 6 ya mwaka 2011, mwanasheria wa tume hiyo, Ali Juma Ali alisema watoto wanazo haki mbalimbali.

Ali alisema mojawapo ni kulindwa, kupewa matibabu, kupatiwa elimu ya lazima, kutoingizwa kwenye ndoa kabla ya wakati na hata suala la kumfundisha maadili na uzalendo wa nchi yake.

Naye sheha wa shehia ya Uwandani, Hamad Ali Mbarouk alisema wamekuwa na ukakasi wa namna ya sheria inavyotaka, iwapo kumejitokeza ubakaji na utiaji mimba kwa mtu aliyevuka miaka 18.

Mkutano huo wa siku moja, ulioandaliwa na Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, ulikuwa na lengo la kutoa elimu kwa makundi kadhaa ya jamii juu ya sheria za elimu, ushahidi, sheria ya mtoto katika vipengele vinavyogusua haki na wajibu wa watoto.

Washiriki wa mkutano huo wa siku moja, walisema bado jamii ya Zanzibar inahitaji elimu ya kila siku, ili izidi kuziheshimu na kuzitekeleza sheria na haki za mtoto