Jaji Mutungi: Namtambua Profesa Lipumba

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi 

Muktasari:

Amesema hana hofu ya kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake.  

Dar es Salaam. Hatimaye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema anamtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif ni Katibu Mkuu.

Amesema hana hofu ya kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja baada ya taarifa na kauli za matusi na kejeli zilizomuhusisha yeye na ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh300 milioni za ruzuku kwenda kwenye akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF ilidai siyo ya chama hicho.  

Taarifa za msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa kwa njia inayoonekana kutia shaka zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alilinganisha suala hilo na uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.