Jaji achukizwa Babu Tale kutotokea mahakamani

Babu Tale 

Muktasari:

Alipaswa kutokea mahakamani kusikiliza uamuzi wa shauri lake kuhusu amri ya mahakama 

Dar es Salaam. Jaji Edson Mkasimongwa wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam amechukizwa na uamuzi wa Mkurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection, Hamis Shaban Taletale maarufu Babu Tale kusafiri nje ya nchi bila taarifa na kushindwa kufika mahakamani.

Babu Tale alitakiwa kufika mahakamani leo Jumatatu Juni 25, 2018 kusikiliza uamuzi wa shauri lake kuhusu  wa amri ya mahakama hiyo kumkamata na kumfunga jela kama mfungwa wa madai.

Hata hivyo hakutokea mahakamani na badala yake alitokea kaka yake, Idd Shaban Taletale huku wakili wao, Issa Chondo akiieleza mahakama kuwa Babu Tale hayuko mahakamani kwa kuwa amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Kitendo hicho cha kusafiri nje ya nchi bila kutoa taarifa kimemuudhi jaji huyo na kubainisha kuwa si cha kiungwana.

Awali wakili Chondo amedai Babu Tale alikwemda Afika Kusini kwa ajili ya matibabu lakini aliponwa maswali na jaji huyo amesema hajui amekwenda nchi gani, kutaka kupewa muda ili kuuliza.

Wakili wa upande wa pili katika shauri hilo, Mwesigwa Muhingo aliingilia kati na kuieleza mahakama kuwa Babu Tale yuko nchini Marekani.

“Alichokifanya si cha kiungwana, alichokifanya si cha kiungwana, alichokifanya si cha kiungwana. Kwa kuwa kesho nasafiri na narudi Jumapili, naamuru tuonane hapa Jumatatu saa 3:00 Asubuhi na yeye (Babu Tale) awepo,” amesema Jaji.