Jaji aeleza utetezi dhaifu ulivyompeleka Lulu jela

Muktasari:

  • Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema kuwa ingawa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ulikuwa ni wa kimazingira, mshtakiwa alikuwa na jukumu la kueleza ni masaibu gani au mazingira gani yalisababisha kifo cha Steven Kanumba kwa kuwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa naye.

Dar es Salaam. Jaji wa Mahakama Kuu, Sam Rumanyika jana ameeleza jinsi ushahidi wa upande wa utetezi ulivyomfanya Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema kuwa ingawa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ulikuwa ni wa kimazingira, mshtakiwa alikuwa na jukumu la kueleza ni masaibu gani au mazingira gani yalisababisha kifo cha Steven Kanumba kwa kuwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa naye.

Alisema kuwa hata hivyo msanii huyo kwa kuwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hakuweza kutoa maelezo ya kujitosheleza hivyo akamtia hatiani kwa kwa kutumia kanuni hiyo mtu wa mwisho kuwa na marehemu kupatikana na hatia asipotoa maelezo ya kuridhisha.

Baada ya Jaji Rumanyika kumtia hatiani msanii huyo, wakili Peter Kibatala alijitahidi kumuombea msamaha ili apunguziwe adhabu huku akiisihi Mahakama imhukumu kifungo cha nje.

Pamoja na mambo mengine Wakili Kibatala alisema kwamba mshtakiwa ni mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo kama ambavyo upande wa mashtaka ulivyosema na kwamba wakati wa tukio hilo alikuwa bado mtoto ambaye alihitaji kuongozwa vema hata na Kanumba.

Wakili Kibatala aliongeza kuwa hata hivyo kwa sasa msanii huyo alishajirerekebisha na kurudi katika mstari na kwamba kwa kuwa ndiye anayetegemewa na mama yake na wadogo zake wengine katika kuwahudumia.

Hata hivyo, utetezi huo hasa wa kuomba afungwe kifungo cha nje haukufanikiwa kwani wakati akitoa adhabu hiyo Jaji Rumanyika licha ya kusema kwamba pamoja na kuzingatia mambo yote hayo, anamhukumu kifungo cha miaka miwili jela.

“Uwezo wa majaji katika kutoa hukumu kimsingi hauna kanuni lakini kuna vitu vya kuzingatia na moja ya vitu hivyo ni kwamba wahalifu kama alivyo mshtakiwa ni zao la jamii,” alisema Jaji Rumanyika na kuongeza:

“Pamoja na mambo mengine Mahakama iliyoyazingatia, ninamhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Kabla ya kufikia hatua hiyo ya kumtia hatiani na kisha kumhukumu adhabu hiyo, Jaji Rumanyika alianza kwa kufanya uchambuzi wa ushahidi wa pande zote na kisha kuainisha udhaifu wa utetezi wa mshtakiwa huyo.

Alisema ushahidi wa upande wa mashtaka ambao ulitolewa na mashahidi wanne ulikwa ni wa kimazingira tu na kwamba hakuna hata chembe ya ushahidi wa moja kwa moja yaani kushuhudia tukio.

Jaji Rumanyika alisema: “Hata yeye mshtakiwa alikiri kuwa ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, ambaye alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne;

Alisema katika ushahidi wa kimazingira isipokuwa mshtakiwa hatatoa maelezo ya kutosheleza kuelezea masaibu au mazingira ya kifo hicho ndo atakuwa na hatia. Hata hivyo alisema msimamo huo wa kisheria hauwezi kuchukuliwa kuwa mshtakiwa ni lazima athibitishe kutokuhusika.

“Ushahidi huo wa kimazingira haumtii hatiani isipokuwa tu kama unaendelea kumnyooshea kidole mshtakiwa kwamba ni yeye pekee ndo alitenda kosa,”

“Nikiangalia maelezo ya mshtakiwa kuona kama yanakidhi viwango shahidi wa kwanza Seth Bosco alisema kile ambacho hata mshtakiwa alikubali kuwa na ugomvi mshtakiwa na marehemu Kanumba.

Alisema kamusi inafafanua kugomba ni patashika baina ya watu wawili huku mmoja aki-resist hiyo hali. Jaji Rumanyika alisema kwa maoni yake hiyo ndio tafsiri ya ugomvi basi mmoja kuanguka ni moja ya mambo yanayotarajiwa au mmoja kumsukuma mwingine;

“Mshtakiwa alisema kuonyesha kuwa marehemu alikuwa mlevi, kama inavyojulikana matokeo ya mlevi ni pamoja na kuanguka. Mshtakiwa ana jukumu la kutoa maelezo ya kujitosheleza lakini alijikanganya;

“Alisema marehemu alimfukuza hadi akamkamata umbali wa zaidi ya mita 27, akafanikiwa kumkamata, kumburuza hadi chumbani. Hakuwahi kusema wakati akimfukuza umbali huo, mlevi huyu alipata kuanguka.|”

Akizungumzia maelezo ya ushahidi wa Josephine Mshumbusi yaliyopokewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa mshtakiwa, Jaji Rumanyika alisema maelezo hayo hayana ushahidi mwingine wa kuyaunga mkono na kwamba hivyo unaacha mashaka.

Alisisitiza kuwa maelezo hayo si cheti cha hospitali na hivyo hayana hadhi ya kuchukuliwa huku akisema kuwa haikuwahi kusemwa kuwa Mshumbusi alikuwa ni mmoja wa madaktari binafsi wa Kanumba, isipokuwa Dk Paplas Kagaiya.

Alisema hata ilitarajiwa kuwa Kagaiya angeeleza historia ya Kanumba (kuhusu kuwa na maradhi ambayo yalielezwa katika maelezo ya Mshumbusi)

Alisema hata mshtakiwa kama mpenzi wa Kanumba kwa miezi hiyo minne kuwa anajua historia hiyo ya marehemu Kanumba lakini naye hakuweza kuyaeleza.

Kuhusu madai ya msanii huyo kupigwa na Kanumba alisema kuwa hilo linakinzana na hekima na busara ya kawaida kwamba hakuthubutu kumrudishia kumpiga wala kumsukuma.

“Ni kama alichukua utaratibu wa kibiblia kwamba anayekupiga shavu la kulia unamgeuzia na shavu la kushoto;

“Nini kilitokea tunabaki na watu wawili tu ama yeye mshtakiwa au marehemu lakini hata marehemu akifufuka Mahakama haitakuwa na mujiza wa kuchukua ushahidi wake;

“Pengine mwingine anaweza kusema kuwa wakati ule mshtakiwa alikuwa na miaka 17 hivyo alikuwa mtoto na alifanya asichokijua. Kesi hii ina mazingira tofauti, mshtakiwa alikuwa mtoto lakini kielelezo kinaonyesha aliitwa mke wa marehemu na akiitika;

“Alikuwa anathubutu kufanya kinyume cha maelekezo ya wazazi wake, mshtakiwa ni aina ya mtoto anayeweza kutoka kwa wazazi wake na kwenda kutembea na wenzake usiku wa manane, anakwenda kwa mpenzi wake, hivyo huyu si yule anayelengwa kulindwa na Sheria ya Mtoto,”alisema Jaji Rumanyika na kuongeza

“Kama mtoto kwa umri anaweza kufanya mambo ya watu wazima ipo siku Mahakama hii itajaa watu wazima waliofanya mambo ya watoto wakaomba kinga ya Sheria ya Mtoto.”

Alisema, “sheria inakusudia kuleta udhibiti wa kufanya mambo yasiyo sawa na inapowezekana kuyafanya yafanywe kwa tahadhari kiasi;

“Itoshe tu kusema kwamba mshtakiwa ameleta utetezi wake marehemu alikuwa na wivu uliovuka mipaka usio na msingi ndo ilipotokea kupigwa.”

Jaji Rumanyika alisema hakuna mchezo usio na kanuni kama mapenzi ni mchezo, wivu ni moja ya kanuni hivyo mshtakiwa hakuwa na chaguo, alishaingia kwenye mchezo huo.

“Bahati mbaya wivu wa kimandeleo huleta maendeleo, wivu wa kimapenzi huleta maangamizi”

“Mshtakiwa alishafahamu marehemu alikuwa na wivu, kama alimfahamu kwa kiwango hicho pia marehemu alipomshuku kwa simu ya kimapenzi hakuacha.”

“Hivyo nalazimika kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya kifungu cha 195 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai.”

Jaji Rumanyika alitumia muda wa dakika 50 kusoma hukumu hiyo kuanzia saa 4:15 alianza kusoma hukumu hiyo kwa kutoa muhtasari wa kesi mpaka saa 5:05, alipotamka adhabu hiyo dhidi ya mshtakiwa.

Hukumu hiyo ilisababisha vilio vya huzuni kwa wazazi, ndugu jamaa na marafiki wa msanii huyo kwa upande mmoja, huku mama wa marehemu Kanumba, Florah Mtegoa akiangua kilio kwa furaha akieleza kuwa Mahakama imetenda haki na kwamba sasa anakwena makaburini kumzika rasmi mwanaye.

Msanii huyo aliondolewa mahakamani hapo kupelekwa gerezani katika gereza la Segerea saa 7:38 kwa kutumia gari la Polisi aina ya Toyota Landcruiser, double cabin.

Wakata rufaa

Muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kumuhukumu Lulu, msanii huyo alianza mapambano upya kuhakikisha anarejea tena uraiani kwa njia ya dhamana na rufaa.

Lulu kupitia kwa mawakili wake alianza mchakato wa kujinasua kutoka katika adhabu hiyo, baada ya kuwasilisha mahakamani hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani.

Mmoja wa mawakili wa msanii huyo, Peter Kibatala alilieleza Mwananchi kuwa hawakuridhika na hukumu hiyo na kwamba tayari waliwasilisha mahakamani hapo taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.

“Tayari tumeshawasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa mahakamani (Mahakama Kuu) hivyo kilichobakia ni process (taratibu nyingine tu za kimahakama,” alisema Wakili Kibatala.

Kibatala alisema kuwa mbali na kukata rufaa pia watawasilisha maombi ya dhamana ili wakati anasubiria usikilizwaji na uamuzi wa rufaa yake akiwa nje.

Taarifa Zaidi

Kanumba alifariki dunia April 7, 2012, kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo wake lijulikanalo kwa kitaalamu kama Brain Concussion, lililosababisha mfumo wa upumuaji kushindwa kufanya kazi.

Alipatwa na tatizo hilo wakati wa ugomvi ulioibuka baina yao usiku huo nyumbani kwake Sinza Vatcan, kutokana na wivu wa kimapenzi, baada ya kumtuhumu mpenzi wake huyo kuongea na simu na mwanaume mwingine.