Tuesday, February 13, 2018

Jaji ataka mashahidi wengi waandaliwe kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya

Askari akiegesha Pikipiki katika Viwanja vya

Askari akiegesha Pikipiki katika Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro mwisho wa wiki. Pikiki hii nimoja ya vielezo katika kesi ya mauwaji ya Bilionea Erasto Msuya. Picha na Dionis Nyato 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto Msuya ameusihi upande wa mashtaka kuhakikisha mashahidi wanapatikana ili kesi isiahirishwe kwa kukosekana shahidi.

Jaji Maghimbi alitoa kauli hiyo jana baada ya shahidi wa 19, Thomas Mosha kumaliza kutoa ushahidi wake saa 7:30 mchana na upande wa mashtaka kueleza hauna shahidi mwingine kwa siku ya jana.

Wakili wa utetezi, John Lundu anayesaidiana na mawakili Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Emmanuel Safari aliiomba mahakama isisikilize ombi la upande wa mashtaka la kutaka kesi iahirishwe. “Kilio cha upande wa mashtaka ni kilekile. Sasa hivi ni saa saba tunaacha kazi, kweli mheshimiwa jaji? Sipendi kurudia yale niliyoyasema Ijumaa lakini naomba mahakama isisikilize hilo ombi,” alisema.

Jaji Maghimbi alimuuliza Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Maugo kama ana lolote la kusema ndipo akasema wao hawana cha kuiambia mahakama zaidi ya kuomba kesi iahirishwe hadi leo.

Ni kutokana na kauli hiyo, Jaji Maghimbi alisema hoja ya upande wa utetezi ina mashiko, hivyo upande wa mashtaka ujitahidi kuandaa mashahidi wa kutosha japo anafahamu ugumu wake.

Awali akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Kassim Nassir, shahidi huyo wa 19, Mosha, alieleza namna alivyoshiriki na watu wengine kutafuta bunduki aina ya SMG.

Baadhi ya mashahidi waliotangulia kutoa ushahidi wao walidai bunduki hiyo ya kivita yenye namba 1952 KJ 10520 ndio ambayo ilitumika kumuua mfanyabiashara huyo Agosti 7, 2013.

Mosha ambaye ni mwenyekiti wa madereva wa bodaboda na mkazi wa Kijiji cha Kyu wilayani Siha aliiambia mahakama kuwa Septemba 11, 2013 alishiriki kutafuta bunduki hiyo katika Ziwa Boloti.

Alisema siku hiyo akiwa kijiweni kwake na madereva wenzake, alifika mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) ambaye hamfahamu jina akitaka wasaidiane na polisi kuisaka bunduki hiyo.

Mosha alisema RCO aliwaeleza kuwa kuna bunduki imefanya uhalifu na imefichwa katika kichaka cha ziwa hilo, hivyo washirikiane na polisi pamoja na wananchi wengine kuitafuta. “Walitupanga katika makundi na tulitafuta kwa kama nusu saa ndipo mzee mmoja anaitwa Joseph (Mushi) alipiga kelele akisema kuna mfuko hapa (wa sandarusi),” alidai shahidi huyo.

“Kulikuwa na polisi hakuwa mbali alivuta ule mfuko akatoa silaha iliyokuwemo ndani. Aliijaribu na kutoa magazine ambayo haikuwa na risasi ndio akatuambia hii ni bunduki aina ya SMG.”

Akihojiwa na wakili Magafu, shahidi huyo alisema baada ya kumaliza kazi hiyo alirudi kijiweni kwake kuendelea na kazi hadi baada ya siku mbili ndipo alipoandikisha maelezo yake.

Alipoulizwa kama maelezo hayo aliyaandikishia kituo cha polisi au eneo gani, alisema polisi walifika katika kijiwe chao na kuwaandikisha maelezo na kwamba anakumbuka hakuyasaini.

Alisema hafahamu kama utaratibu wa polisi ni lazima asaini maelezo yake baada ya kumaliza kuyatoa zaidi ya kusema alivyomaliza alibeba begi lake na kuondoka eneo hilo.

Alipoulizwa kama anajua ni nani aliiweka bunduki hiyo katika eneo hilo na ilitumika katika uhalifu gani, shahidi huyo alisema hamfahamu na wala hajui ilitumika katika tukio gani la uhalifu.


-->