Jalada kesi ya kina Ringo Tenga latua kwa DPP

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wanne wa Kampuni ya Six Telecoms, akiwemo Dk Ringo Tenga, limetua mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa ajili ya kulipitia.

 

Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa upelelezi wa shauri hilo pamoja na zoezi la uchapaji wa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

 

Hayo yalielezwa leo Ijumaa Juni 23, 2018 na wakili wa Serikali,  Jacquline Nyatore katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa.

 

Nyantore amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa jalada la shauri hilo limeshakamilika kuchapwa na sasa limepelekwa kwa DPP kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.

 

"Tarehe ijayo nitakuja na maelekezo ambayo nitakuwa nimepewa na DPP," amedai wakili Nyantore.

 

Awali, wakili wa utetezi, Bryson Shayo ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha tarehe itakayopangwa na mahakama, waje na kitu kipya ili kesi hiyo iweze kuendelea kwa sababu ni shauri la muda mrefu.

 

Baada ya maelezo hayo, hakimu Simba ameiahirisha kesi hiyo hadi Julai 6, 2018 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

 

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni mhandisi Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni wa hiyo, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni na mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

 

Dk Ringo ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanakabiliwa na mashitaka sita yakiwemo ya utakatishaji wa fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.