Jamii yakumbushwa kusaidia wenye uhitaji

Muktasari:

Wito huo umetolewa na mlezi wa Hospitali ya Tumbi wakati akipokea misaada kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Safi

Kibaha. Jamii imetakiwa kuwa na utaratibu wa kujitolea kwa watu wenye mahitaji maalum ili kueneza upendo kwa wasio na uwezo kujiona wako sawa.

Wito huo umetolewa leo Augusti 19, 2018 na mlezi wa Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha mkoa wa Pwani, Robby Mosses wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa shule ya msingi na awali ya Safi School iliyopo Mbezi Makabe, Dar es Salaam.

Akipokea bidhaa hizo zikiwamo sabuni na mafuta, Mosses amesema bado kuna uhitaji kwa kuwa wanapokea wagonjwa wengi wenye kuhitaji na wakiwa na hali mbaya.

"Kama jamii ina uwezo na nafasi wajitokeze walete bado kuna uhitaji wa vitu mbalimbali,” amesema Mosses

Amesema wanapokea majeruhi wengi wanaohitaji msaada hivyo kuwashukuru watoto na uongozi wa Safi School kwa kuliona hilo na wengine wajitokeze.

Kwa upande wake, meneja wa shule hiyo, Jackson Mfuru amesema ni utaratibu wao ambao wameuanza kwa kuwafundisha watoto upendo kwamba wanatakiwa kutoa na kuwajali watoto wenzao kwa hali na mali ili kufarijiana katika shida na raha.

Ameahidi kujikusanya na kuendelea kufanya hivyo huku akiwataka wanafunzi na taasisi nyingine kuwa na utaratibu huo kwa lengo la kusaidiana katika jamii.

Naye mgonjwa aliyekuwa amelazwa na mtoto Prisca Hamza huku akifurahia upendo huo aliushukuru uongozi wa shule kwa zawadi hizo kwao kwani ni sehemu ya kufundishwa upendo na kuishi na wenzao wenye hali zote.

Akizungumza kwa niaba ya watoto wenzao, mtoto wa darasa la sita, Blisse Mwarabu amesema wamefarijika kuona watoto wenzao licha ya kwamba wapo katika hali ya ugonjwa na kuwaombea wapone haraka.