Je, Sheng nchini Kenya ni vurugu za kimawasiliano?

Muktasari:

Mjadala huo unahusiana na masuala makubwa kadha kuhusu lugha hiyo: Mosi, ikiwa Sheng ni lugha au si lugha. Pili, Sheng inajadiliwa kuwa sababu ya kifo cha lugha ya Kiswahili nchini Kenya, na tatu kuna mjadala unaoendelea kuwa Sheng ni fujo au vurugu tu za kimawasiliano, kwa sababu ya kubadilikabadilika kwake na kuyatenga baadhi ya makundi ya watumiaji wa lugha za Kiswahili na Kiingereza pindi inapotumika.

Kumekuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wasomi katika Afrika Mashariki na kwingineko mintarafu matumizi ya ‘lugha’ ijulikanayo kama Sheng huko nchini Kenya.

Mjadala huo unahusiana na masuala makubwa kadha kuhusu lugha hiyo: Mosi, ikiwa Sheng ni lugha au si lugha. Pili, Sheng inajadiliwa kuwa sababu ya kifo cha lugha ya Kiswahili nchini Kenya, na tatu kuna mjadala unaoendelea kuwa Sheng ni fujo au vurugu tu za kimawasiliano, kwa sababu ya kubadilikabadilika kwake na kuyatenga baadhi ya makundi ya watumiaji wa lugha za Kiswahili na Kiingereza pindi inapotumika.

Kutoka ndani na nje ya Kenya, wapo wanaoichukulia ‘lugha’ hiyo kwa mtazamo chanya kwamba ina mustakabali mwema katika maendeleo ya lugha hususan ya Kiswahili na uga wa mawasiliano kwa ujumla.

Hata hivyo, wapo pia waonao kuwa Sheng haina mustakabali wa kujenga bali kubomoa tu Kiswahili na Kiingereza pia.

Godfrey Kariuki, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, akiwasilisha mada yake: “Je, Sheng ni lugha ya kuvutia au ni kifo cha Kiswahili?” katika jopo la wajuzi na wanafunzi wa kigeni wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Humboldt Berlin, nchini Ujerumani, hivi karibuni alitoa mtazamo wa watu nchini Kenya kuhusu ‘lugha’ hiyo.

Anaeleza; “Sheng kama lugha ina misingi ya sarufi ya Kiswahili lakini imekopa maneno mengi kutoka Kiingereza na lugha nyingine za Kenya kama vile Kijaluo, Kikikuyu, Kiluhya, Kitaita na kadhalika.” Kariuki anaendelea kueleza kuwa Sheng inatumika zaidi Nairobi, Mombasa na Nakuru.

Mbali ya Sheng kutumiwa zaidi na kundi la vijana, inatumiwa pia na watu wa tabaka la chini waishio ‘madongoporomoka’ kama vile Kaloleni na Dandora, yaani eneo la Eastlands la Nairobi kwa ujumla. Sheng hupendwa pia na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya na watungaji wa mashairi.

Hata hivyo, Kariuki anabainisha kuwa ‘lugha’ hii inawachukiza walimu na wale wanaouenzi usanifu wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Mwalimu Mercy Maloba kutoka Nairobi, akichangia katika mjadala huo anaeleza kuwa lugha hiyo ina mchango mkubwa katika kuporomosha umakini wa wanafunzi dhidi ya uelewa wa lugha hizo.

Anaeleza: “Ufundishaji wa lugha kwa wanafunzi umekuwa mgumu zaidi, sasa hawawezi kuongea Kiswahili wala Kiingereza kwa mfululizo. Huchanganya lugha bila utaratibu...”

Naye Daniel Nyamboga, kutoka Chuo Kikuu Nairobi, anapinga kabisa matumizi ya Sheng. Anayaona kuwa ni fujo katika mawasiliano na kwamba ni uharibifu wa Kiswahili.

Pamoja na mitazamo mbalimbali kuhusu matumizi ya Sheng, wataalamu katika uga wa isimu jamii, wanaichukulia ‘lugha’ hiyo kama utajiri katika maendeleo ya lugha.

Inaelezwa kuwa, mitindo ya mawasiliano kama ilivyo misimu inayoibuka nje ya matumizi rasmi ya lugha fulani, ina mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha kama vile Kiswahili.

Mitindo hiyo huwasaidia watumiaji kukidhi haja ya mawasiliano baina yao, huwawezesha kutunza faragha katika mawasiliano. Hata baadhi ya maneno yatumikayo katika mitindo hiyo isiyo rasmi ya kuwasiliana, ina mchango mkubwa katika lugha rasmi, kwa kuwa maneno yake huweza kusanifishwa na kuingizwa katika orodha ya msamiati wa lugha husika. Katika mtazamo huu, jambo linalosisitizwa ni kwamba, walimu waweke msisitizo mkubwa na umakini katika ufundishaji wa lugha za hizo.