Jela miaka 7 kwa kipigo kilichomng’oa mtoto meno

Muktasari:

  • Licha ya kumpiga ngumi mtoto wake, Sumila pia alimpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili baada ya kupewa taarifa kwamba mtoto wake huyo alikuwa ni mtoro shuleni na alishapewa onyo la utoro shuleni hapo.

Dar Es Salaam. Mkazi wa Ukonga Mazizini, Elihsa Sumila (35) amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na hatia ya kumjeruhi mtoto wake wa kumzaa kwa kumpiga ngumi ya mdomo na kumng’oa meno mawili.

Licha ya kumpiga ngumi mtoto wake, Sumila pia alimpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili baada ya kupewa taarifa kwamba mtoto wake huyo alikuwa ni mtoro shuleni na alishapewa onyo la utoro shuleni hapo.

Mshtakiwa huyo amehukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada mahakama hiyo kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano akiwemo daktari.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo John Msafiri alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na hivyo anamtia hatiani kama alivyoshtakiwa na kwamba Sumila atatumikia kifungo cha miaka saba jela.

“Baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka nimejiridhisha pasi kuacha shaka kuwa mshtakiwa alimjeruhi mtoto huyu na kumsababisha majereha” alisema hakimu Msafiri.