Friday, April 14, 2017

Jengo la NBS Dodoma kugharimu Sh11.6 bilioni

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Dodoma. Katika kutii agizo la Rais John Magufuli la kuhamia Dodoma, Ofisi za Taifa za Takwimu (NBS) zimeanza ujenzi wa jengo la ghorofa tano mkoani humo zitakazogharimu Sh11.6 bilioni.

Imeelezwa ofisi hizo zitarahisisha usimamizi wa takwimu kwenye mikoa yote nchini.

Akizungumza jana baada ya ukaguzi wa msingi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema Kampuni ya Hainan International Ltd ya China ndiyo iliyopewa kazi ya kujenga jengo hilo.

Alisema jengo hilo linalojengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) lipo katika eneo la NCC jirani na makao makuu ya Hazina.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutamaliza changamoto za ufinyu wa ofisi uliopo kwenye makao makuu ambayo kwa sasa yapo Dar es Salaam.

“Ninakagua ujenzi wa ofisi zetu kwa sababu sisi ni miongoni mwa wanaotakiwa kuhamia Dodoma kutii agizo la Rais John Magufuli,” alisema.

Dk Chuwa alisema ameridhishwa na namna ujenzi huo unavyoendelea na akaagiza ukamilike katika kipindi walichokubaliana kwenye mkataba.

“Kama wenzetu Uganda wamejenga jengo la takwimu la ghorofa 12 kwa mwaka mmoja iweje sisi tutumie mwaka mmoja kujenga ghorofa tano, ikiwezekana jengo likamilike kabla ya muda uliopangwa,” alisema.

Mtumwa Shomvi, ambaye ni Mshauri Mkuu wa mradi huo kutoka Kampuni ya Y&P Archtect Ltd alisema mradi huo utamalizika kwa viwango na muda uliopangwa.

Msimamizi wa ujenzi wa Kampuni ya Hainan International Ltd, Lan Shuiqing alisema jengo hilo litakamilika kwa wakati.

“Kampuni yetu ina uzoefu katika masuala ya ujenzi, tumefanya hivyo kwenye nchi mbalimbali hatubahatishi,’’ alisema.

-->