Jeshi Zimbabwe lamkingia kifua makamu wa rais

Muktasari:

  • Mchakato wa sasa wa kuwaondoa na kuitakasa Zanu-PF ambao kwa sasa unawalenga zaidi wanachama waliohusika na historia ya ukombozi wetu unatupa shida sana sisi tulioko kwenye vikosi vya ulinzi.
  • Tunawakumbusha wale wanaofanya hivyo kwamba linapokuja suala la kulinda uhuru wetu jeshi halitasita kuingilia kati.

Harare, Zimbabwe. Imeripotiwa kwamba Zimbabwe “iko ukingoni” baada ya Mkuu wa Jeshi Jenerali Constantino Chiwenga kuagiza “kusitishwa” ufukuzaji wanachama kutoka chama cha Zanu PF cha Rais Robert Mugabe kufuatia kufutwa kazi kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.

Jenerali Chiwenga akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na walau makamanda 90 wa ngazi ya juu kwenye makao makuu ya jeshi, Jumatatu alisema: "Ufukuzaji huu unaolenga wanachama wa chama wenye uhusiano na harakati za ukombozi lazima ukome mara moja."

Kwa mujibu wa mtandao wa New Zimbabwe.com, Jenerali Chiwenga aliporejea nchini hivi karibuni akitokea China alikuta Mnangagwa amefutwa kazi serikalini na amefutiwa uanachama Zanu-PF.

Ripoti zinasema kwamba jeshi limekuwa likimuunga mkono Mnangagwa kumrithi Mugabe, 93, lakini mke wa mzee huyo Grace ameibuka na kuwa mshindani mwenye nafasi kubwa.

Mnangagwa alifukuzwa serikalini na kwenye chama wiki iliyopita baada ya kushutumiwa kwamba alikuwa anapanga njama za kumwondoa mamlakani Mugabe. Mnangagwa amekimbilia uhamishoni.

Jenerali Chiwenga amekishutumu chama kwa uamuzi wa kuwafukuza maofisa waandamizi walioshiriki, miaka ya 1970, vita dhidi ya wazungu wachache walioitawala Rhodesia, Zimbabwe ya leo akisema "mapinduzi kinzani" yanaandaliwa kukiharibu chama.

"Mchakato wa sasa wa kuwaondoa na kuitakasa Zanu-PF ambao kwa unawalenga zaidi wanachama waliohusika na historia ya ukombozi wetu unatupa shida sana sisi tulioko kwenye vikosi vya ulinzi," alisema Chiwenga huku akisoma taarifa iliyoandaliwa.

“Tunawakumbusha wale wanaofanya hivyo kwamba linapokuja suala la kulinda uhuru wetu jeshi halitasita kuingilia kati. Mchakato huu wa kuondoa watu kwa kulenga wanachama wenye uhusiano na harakati za ukombozi lazima ukome mara moja,” alisisitiza.