Jinamizi la ajali lawakutanisha viongozi, waiombea Mbeya

Machifu wa kimila Mkoa wa Mbeya, wakiongozwa na Chifu Mkuu, Roketi Mwashinga (katikati mwenye rasta) wakiwa kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya kwa ajili ya kuungana na viongozi wa Serikali ya Mkoa huo, viongozi wa dini zote na wananchi kwa ajili ya kufanya maombi maalumu ya kuuombea mkoa ili kuepukana na matukio ya ajali. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Baadhi ya viongozi walioshiriki ibada ya maombi ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson


Mbeya. Viongozi wa dini, Serikali na kimila wakiwa sambamba na wananchi leo Alhamisi Julai 12, 2018 wamejitokeza katika viwanja vya Ruanda Nzovwe mjini hapa kwa ajili ya  kuombea Mkoa wa Mbeya kutokana na mfululizo wa ajali ndani ya mwezi mmoja.

Juni 14, 2018 watu 13 wakiwemo vijana 10 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ofisa mmoja wa JWTZ, dereva na kondakta wake walifariki dunia.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Kambi ya JKT-Itende Kikosi cha 844KJ-Itende kwa mafunzo ya vitendo kupinduka eneo la mteremko wa Mwase jijini Mbeya barabara ya Mbeya mjini-Chunya.

Ajali nyingine ni ile ya Julai Mosi, 2018 watu 20 walifariki papo hapo na wengine 45 kujeruhiwa baada ya lori kugonga mabasi matatu madogo ya abiria kwenye mteremko wa Mlima Iwambi-Mbalizi wilayani Mbeya katika barabara ya Tanzania-Zambia.

Kufuatia hali hiyo, viongozi wamefanya ibada ya maombi na leo walioshiriki ibada hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla; Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na Naibu Waziri wa Kilimo, Dk Mary Mwanjelwa.

Kabla ya kuanza ibadi hiyo, kwaya mbalimbali za mkoani hapa ziliimba nyimbo za kuabudu.

Baadhi ya kwaya hizo ni kwaya ya bikira maria usharika wa Ruanda na ile ya Paradise.

Soma Zaidi: