Jinamizi la siasa latesa urais Daruso

Muktasari:

  • Hata hivyo, siasa zinazotajwa kukinyima chombo hicho uongozi wake wa juu mpaka sasa ni za vyama vya CCM na Chadema.

Dar es Salaam. Ni siasa tu zinazoinyima rais Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso). Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya uchaguzi uliofanyika Mei 23, ambao ulimpata kiongozi wa juu wa chombo hicho cha wanafunzi kukwama.

Hata hivyo, siasa zinazotajwa kukinyima chombo hicho uongozi wake wa juu mpaka sasa ni za vyama vya CCM na Chadema.

Mei 24, uongozi wa chuo hicho ulisitisha mchakato wa kuapishwa kwa rais mpya wa Daruso, Harun Stanley ambaye alitangazwa kushinda Mei 23.

Mchakato huo ulisitishwa baada ya uongozi wa chuo kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wawili wakidai uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Akizungumza na Mwananchi Juni 23, Stanley alisema hana anachofahamu zaidi ya barua iliyoandikwa na uongozi wa chuo hicho mara ya mwisho.

“Sifahamu nini kinaendelea, mara ya mwisho uongozi wa chuo uliandika barua ya kueleza kuwa wanasubiri ushauri kutoka kwa mwanasheria mkuu wa chuo. Inawezekana wamekaa kimya kutokana na misiba iliyotokea siku za hivi karibuni, ila bado nafuatilia kujua nini kinaendelea, ” alisema Stanley.

Mshauri wa wanafunzi wa UDSM, Paulina Mabuga alipoulizwa kuhusu hatima ya uchaguzi huo, alitaka aulizwe msemaji wa chuo.

Akizungumza na Mwananchi juzi, ofisa uhusiano wa Umma UDSM, Jackson Isdory alisema hakuna kitu kipya zaidi ya barua iliyokuwa na maelezo ya kutosha.

“Barua ilijieleza kuwa uongozi wa chuo unasubiri kupata ushauri kutoka kwa mwanasheria mkuu wa chuo, hilo ndilo lililopo,” alisema Isdory.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa ‘figisu’ za uchaguzi wa Daruso zimetokana na kuingiliwa na siasa za Chadema na CCM, ambapo kila chama kinadaiwa kuwa na mgombea wake.

Jinamizi la uchaguzi huo lilianza siku chache kabla ya Mei 23, baada ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi chuoni hapo, Kambarage Kinemo na katibu wake, Ishengoma Ladislaus kukamatwa wakituhumiwa kwa wizi wa simu.

Licha ya uchaguzi huo kufanyika Mei 23, siku chache baadaye kabla ya kuapishwa kwa rais mpya, uongozi wa chuo ulisitisha mchakato huo.

Baadaye kiliitishwa kikao kilichozikutanisha pande mbili; uongozi wa chuo na Daruso, lakini walishindwa kufikia muafaka baada ya mshauri wa wanafunzi, Paulina kutoka nje ya kikao.

Awali, Kinemo alipoulizwa kuhusu kuvunjika kwa mkutano huo alisema walikutana kuzungumzia rufaa, lakini ulitokea mkanganyiko uliomfanya mshauri wa wanafunzi kuondoka.

Kwa mujibu wa kanuni za Daruso, mshauri wa wanafunzi anapotoka nje ya kikao chochote inamaanisha kuwa kitakuwa kimekwisha, lakini wao wanasubiri maelekezo mengine.

Wakizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi na wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James walikana vyama vyao kujihusisha na siasa ndani ya jumuiya za wanafunzi vyuoni.