Jinsi Magufuli alivyowakimbiza majangili

Muktasari:

Uchambuzi wa takwimu kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) unaonyesha kuwa katika hifadhi 16, matukio ya ujangili yamepungua takriban mara nne, kutoka matukio 8,631 mwaka 2014/15 hadi 2,179 Desemba mwaka jana.

Vita dhidi ya ujangili iliyokolezwa na Rais John Magufuli imeanza kuzaa matunda baada ya matukio ya ujangili kupungua kwa kasi, sambamba na nyara zinazokamatwa, kitu kinachopashiria ufanisi katika kupambana na tatizo hilo.

Uchambuzi wa takwimu kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) unaonyesha kuwa katika hifadhi 16, matukio ya ujangili yamepungua takriban mara nne, kutoka matukio 8,631 mwaka 2014/15 hadi 2,179 Desemba mwaka jana.

Sehemu kubwa ya mafanikio hayo imeonekana mwaka 2015/16 baada ya matukio ya ujangili kushuka katika robo tatu ya hifadhi zote kasoro za Rubondo, Saadani, Kitulo na Mkomazi.

Uchunguzi wa Mwananchi katika baadhi ya hifadhi za Serengeti na Manyara umabaini kuwa baadhi ya watu wameachana na ujangili kwa kuhofia kukamatwa na askari wa kikosi maalum cha kupambana na vitendo hivyo.

Sanjari na doria hizo, mamlaka zinaeleza kuwa ujangili umepungua kutokana na matumizi ya mfumo mpya wa kukabiliana na majangili unaoitwa “ngazi tano” ambao miongoni mwa mbinu zake ni kuvunja mtandao wa watakatishaji fedha ambazo hutumika kuwalipa majangili.

Kupungua kwa matukio hayo ya ujangili ni ahueni kwa wanyamapori baada ya vitendo hivyo kukithiri miaka ya hivi karibuni na kuongeza tishio la kutoweka kwa baadhi ya wanyama adimu ulimwenguni, kama tembo na faru weusi.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songoro anasema moja ya kichocheo cha mafanikio hayo ni ushirikiano mkubwa wa Dk Magufuli, Waziri Profesa Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milanzi na kuanza kutumika mkakati wa kupambana na mtandao wote wa ujangili.

Kabla ya kuingia madarakani, Rais aliahidi kukabiliana na ujangili nchini huku akieleza kuwa yupo radhi kila tembo alindwe na askari mmoja kuokoa wanyama hao. Baada ya kuingia Ikulu Novemba 5, 2015 Dk Magufuli alimteua Milanzi, ambaye ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili ahakikishe anatumia mbinu za chombo hicho cha ulinzi kukomesha ujangili.

Profesa Songoro anasema kikosi kazi cha kupambana na ujangili kilikamata watuhumiwa 5,752 kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na ndani ya kipindi hicho kesi 2,338 zimefikishwa mahakamani.

Operesheni hiyo pia, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, ilifanikisha kukamatwa kwa pembe 4,274 zenye uzito wa kilo 12,333, ambao ni wastani wa pembe 1,430 kwa mwaka.

Ndani ya kipindi hicho, takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2013/14 ndiyo ulikuwa hatari kwa wanyamapori baada ya shehena ya pembe 2,733 kukamatwa kutoka kwa watuhimiwa 1,298.

Ukamataji wa watuhumiwa haukuwa rahisi. Sehemu kubwa ya majangili hutumia silaha kali ambazo ni rahisi kuua wanyama wakubwa kama tembo kwa risasi moja.

Katika mapambano hayo na majangili, Serikali ilikamata bunduki 399, risasi 382 zikiwepo magazini mbili za SMG. Mbali na bunduki, pia ilikamata silaha za jadi 67 na nyara nyingine kama nyamapori tani 3.7.

“Mafanikio haya yanatokana na dhamira ya dhati ya serikali kutokomeza ujangili, kutekelezwa mpango wa kupambana na ujangili wa mwaka 2014/19, kuongeza ushirikiano na nchi jirani katika kupambana na ujangili, kusainiwa kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo pamoja na mambo mengine inadhibiti biashara ya pembe za ndovu,” anasema Profesa Songoro.

Pamoja na ujangili kupungua ndani ya hifadhi 16 za Taifa, takwimu za Tanapa zinabainisha kuwa bado kuna hifadhi tano zinazoongoza kwa matukio hayo, ikiwemo Serengeti, zinazoonekana kushambuliwa zaidi na majangili.

Takwimu za Tanapa zinabainisha kuwa kati ya Julai na Desemba mwaka jana, Serengeti ndiyo ilikuwa ikiongoza kwa ujangili kwa kuwa na matukio 570 ikifuatiwa na Rubondo iliyokuwa na matukio 391.

Kiwango hicho cha ujangili ni kidogo mara nne ya ilivyokuwa mwaka 2014/15 wakati yaliporipotiwa matukio 2,272 ya ujangili. Hata hivyo, bado ni kikubwa ikizingatiwa ni nusu mwaka kikizidi kile cha mwaka 2015/16 kuliporipotiwa matukio 298.

Wakati hifadhi hizo zikiwa na kiwango kikubwa cha vitendo hivyo, zipo baadhi zenye kiwango kidogo cha ujangili kama Saanane iliyoanzishwa hivi karibuni ambayo haijawahi kurekodi tukio la ujangili.

Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Tanapa, Mtango Mtaiko anasema pamoja na Serengeti kuongoza kwa matukio ya ujangili, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hali imeanza kuimarika.

“Hifadhi za Saanane na Gombe zipo salama zaidi kutokana na kuwa kisiwani hivyo imekuwa ni vigumu kwa majangili kuingia na kufanya uhalifu, tofauti na hifadhi ambazo zinazungukwa na makazi ya watu, kama ilivyo Hifadhi ya Serengeti,” alisema Mtaiko.

Hata hivyo, anasema uwepo wa ujangili Hifadhi ya Gombe umetokana na raia kutoka nchi jirani, ambao mara nyingi hukamatwa baada ya kuingia nchini, kufanya uhalifu mdogo kama uvuvi haramu na kukata miti eneo la hifadhi.

Mhifadhi wa Taifa wa Hifadhi ya Serengeti, William Mwakilema alikiri kuendelea kuwepo kwa matukio ya ujangili katika hifadhi hiyo, lakini akasema mengi kwa sasa hayahusishi uuaji wa tembo.

Mwakilema anasema miongoni mwa mikakati wanayotumia kudhibiti ujangili ni pamoja na kushirikisha polisi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuwa na kikosi maalum cha intelejensia na kuimarisha ulinzi.

“Tumekuwa tukifanya kazi kubwa kudhibiti ujangili. Kuna wakati tumeingia kukamata majangili mpaka wa nchi jirani ya Kenya baada ya kukimbilia huko. Tulishirikiana na askari wa Hifadhi ya Masai Mara na maeneo mengine,” alisema.

Tofauti na miaka ya nyuma, mwandishi wetu aliyeshiriki doria kwa usiku mmoja katika hifadhi ya Manyara, alishuhudia askari hao wakingia kwa zamu kufanya doria ili kutotoa mwanya kwa majangili.

Ili kuwa na rekodi nzuri za majangili, mamlaka imetengeneza kanzidata ya watu walioachana na vitendo hivyo.

Mhifadhi mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Dk Noelia Myonga anasema wamewaweka watu walioacha ujangili katika kanzidata kwa kuwa ni wasiri wao wazuri wa kutoa taarifa kabla ya kufanyika ujangili na hata unapofanyika na hivyo kuwawezesha kuwakamata watuhumiwa.

“Hifadhi zimekuwa zikitoa fedha, kuwalipa wasiri hao kama motisha na wengi wamekuwa na msaada mkubwa katika kusaidia vita dhidi ya ujangili,” alisema Dk Myonga.

Mbali na kutumia vikosi vya kiusalama kukabiliana na ujangili, Dk Myonga anasema wananchi wamewasaidia kupunguza vitendo hivyo baada ya wengi kufahamu umuhimu wa utunzaji rasilimali hizo.

“Wananchi wengi wanatupa ushirikiano na hasa kutokana na uwepo wa miradi ya ujirani mwema na kwa ushirikiano na taasisi nyingine kama Frankfurt Zoological Society tumeanzisha benki za vijiji na vikundi vya ujasiriamali,” anasema.

Joram (tumetumia jina la kubuni kwa kuwa ni mmoja wa watoaji taarifa), ambaye ni mkazi wa Mto wa Mbu, anakiri kuwahi kushiriki vitendo vya ujangili na hata kufungwa, lakini sasa amekuwa anasaidiana na askari wa hifadhi kupambana na ujangili.

“Nilifanya ile kazi nikiwa sina uelewa, lakini baada ya kumaliza kifungo nimeona ni bora nilishirikiane na Serikali kupambana na ujangili kwa kuwa ni kweli una faida kubwa kwa taifa letu,” alisema.

Njia mpya ya kuthibiti ujangili

Serikali inaamini kuwa mfumo wa ngazi tano ulioanza kutumika nchi nzima Julai mwaka jana utasaidia kwa kiwango kikubwa kuzuia ujangili.

Elisante Ayoub, mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Hifadhi ya Taifa ya Manyara anasema awali ilikuwa jangili akikamatwa wanamfikisha mahakamani na anafungwa ama kupigwa faini, jambo ambalo alisema halikuwa linasaidia kwa kuwa aliacha mtandao wake nje.

“Lakini kwa sasa tukimkamata jangili, anabanwa ataje mtandao wake wote kwa kutumia mbinu zilizoainishwa kisheria,” anasema bila kuziweka bayana.

Ngazi ya kwanza ya udhibiti, anasema huanza na baadhi ya watu wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi, watumishi wasio waaminifu na watu wengine wanaosaidia ujangili kwa kujua ama kutojua.

Katika ngazi ya pili, mamlaka huwabaini na kuwakamata, mafundi wa utunguaji wanyamapori ambao wamekuwa wakikodiwa kutoka maeneo mbalimbali kwenda kuua wanyama.

Ayoub anasema ngazi ya tatu inajumuisha kundi ambalo limedhibitiwa na lilikuwa hatari katika ujangili ambalo ni la wasafirishaji na madalali wa kuuza pembe za ndovu na maliasili nyingine.

“Kundi la nne tunalodhibiti ni lile linalowezesha mtandao wa ujangili likihusisha waajiriwa wa mawakala wenye mawasiliano moja kwa moja na wapangaji wa mipango na wawezesha wa ujangili,” alisema.

“Ngazi ya mwisho inahusisha kundi linalohusisha watakatishaji fedha, wanaowasiliana na mawakala wa nje ya nchi, wafadhili wa magenge ya uhalifu na wanaopokea maelekezo kutoka nje ya nchi,” anasema Ayoub.

Licha ya kuwa katika hatua changa, mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Robert Mande anasema mfumo huo tayari unafanya kazi katika kanda tisa nchini, hasa maeneo ya Ikolojia kama Serengeti, Tarangire, Manyara na Ngorongoro.

Mengine ni hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ikolojia za Mkomazi, Ruaha /Rungwa, Selous Kusini na Selous Kaskazini, Moyowosi, Katavi na ikolojia ya Burigi, Biharamro na Ibanda.

“Katika maeneo haya tisa ya ikolojia, Selous Kusini ndiyo inayoongoza kwa matukio ya ujangili na eneo ambalo matukio yamepungua sana ni Tarangire, Manyara na Ngorongoro ambako mpango ya ngazi tano ulianzia,” alisema Mande.

Katika kipindi cha mwezi Agosti 2016 hadi Januari mwaka huu, majangili 906 walibainika na kati yao 310 wamekamatwa kwa kutumia njia hiyo na wengine wanaendelea kusakwa.

Kabla ya kuanza kutumika mwaka jana, mfumo huo ulitumika kwa majaribio katika operesheni tokomeza mwaka 2013 na Serikali inasema ulifanikiwa sana kupambana na ujangili, licha ya operesheni hiyo kupingwa na wadau wengi kutokana na namna ilivyoendeshwa.