Jinsi jinamizi la ajali linavyolitafuna Taifa

Muktasari:

  • Miongoni mwa ajali hizo ni ile ya Juni 16 iliyosababisha vifo vya watu 13, wakiwamo vijana kumi na moja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wakitoka Tabora kwenda kambi ya Itende, Mbeya.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) linazitaja ajali za barabarani kama moja ya sababu zinazochangia vifo vingi duniani. Kwa Tanzania, ukweli huo unadhihirishwa na taarifa za vifo vya watu 30 katika matukio ya ajali ndani ya siku 12 kuanzia Juni 6 hadi 18.

Miongoni mwa ajali hizo ni ile ya Juni 16 iliyosababisha vifo vya watu 13, wakiwamo vijana kumi na moja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wakitoka Tabora kwenda kambi ya Itende, Mbeya.

Ajali nyingine ilitokea Juni 6, wakati Basi la Ramada lilipogonga treni eneo la Gundu, Kigoma Ujiji na kusababisha vifo vya watu 12. Aidha, Juni 18 ajali nyingine ilisababisha vifo vya watu watano mkoani Geita na kujeruhi 36. Siku hiyohiyo, basi lililokuwa na abiria 44 lilinusurika kuzama katika Ziwa Victoria katika eneo la Kigongo Feri, Mwanza na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Akizungumzia hali ya ajali nchini Aprili 3, bungeni Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba alisema kuanzia Januari hadi Februari zilisababisha vifo vya watu 334.

Licha ya ajali Juni, Mei pia kulikuwa na matukio kadhaa ya ajali ikiwamo ile iliyoua maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), eneo la Chalinze mkoani Pwani iliyotokea Mei 22.

Pia, Mei 30 watu tisa wakiwamo watoto sita walifariki katika ajali ya gari mkoani Tanga siku moja baada ya ajali iliyohusisha pikipiki na basi iliyoua watu watatu wa familia moja; baba, mama na mtoto eneo la Munio wilayani Sumbawanga.

Naibu waziri wa Afya, Faustine Ndugulile akizungumzia athari za matukio hayo alisema, “Ajali zimekuwa nyingi, vifo hivyo hupoteza nguvu kazi na majeruhi huhitaji huduma za hospitali ambazo ni gharama.”

Dk Ndugulile alisema ajali zinasababisha ongezeko kubwa la watu wanaotaka kupata huduma za afya na aghalabu matibabu ya majeruhi wa ajali ni ya muda mrefu.

“Mfupa kuunga ni miezi mitatu hadi minne, kwa hali hiyo Hospitali ya Taifa Muhimbili, wodi imejaa waathirika wa ajali ambao wanakaa muda mrefu, Serikali inatumia fedha nyingi kwa majeruhi. Hii ni gharama kubwa na sasa tumeanzisha huduma ya kuweka chuma kwenye mfupa,” alisema.

Kwa maoni yake, chanzo kikubwa cha ajali ni ukosefu wa nidhamu, uzembe na ulevi akisema ajali zilizotokea ndani ya siku 12 huenda zimesababisha vifo vingi kuliko hata kipindupindu, Ukimwi, malaria au kisukari.

Kuhusu chanzo cha ajali, Dk Ndugulile aliungwa mkono na ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Tabora, Joseph Michael ambaye alisema asilimia 76 ya ajali za barabarani hutokana na makosa ya kibinadamu akibainisha kwamba asilimia 40 hutokana na uzembe wa madereva.

Kuhusu mikakati ya kukabiliana na ajali, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Fortunatus Muslim alisema kazi kubwa imefanyika na zinaendelea kupungua kutokana na askari wa kikosi hicho kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa sheria katika barabara zote.

“Kwa magari yanayosafiri (ya abiria), ukaguzi unafanyika kabla hayajatoka vituoni na madereva tunawapima ulevi, huko njiani askari nao wanajipanga vizuri,” alisema.

“Hatuwezi kuvumilia watu wapoteze maisha sababu ya madereva wazembe, hatutafungua ‘tuition’ barabarani ya kutoa elimu. Kama unataka elimu acha gari lako nyumbani ukija nalo barabarani na ukavunja sheria neno ni moja tu kamata.”