Joel Bendera azikwa, Joyce Mmasi aagwa Dar

Waandishi wa habari wakiwa wenye simanzi wakipita pembeni mwa jeneza lenye mwili mwandishi mwenzao Joyce Mmasi  walipokuwa wakitoa heshima za mwisho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Rais John Magufuli aliwakilishwa na waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo. Pia, yalihudhuria na katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi; waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na; waziri wa ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

 Wakati Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiungana na waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera mjini Korogwe, mamia ya watu jijini Dar es Salaam jana waliuaga mwili wa mwandishi wa habari mwandamizi, Joyce Mmasi. Mazishi ya Bendera yalifanyika kwenye makaburi ya Kanisa la Anglikana Korogwe mkoani Tanga.

Ibada ya mazishi iliongozwa na Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Tanga, William Mndolwa.

Rais John Magufuli aliwakilishwa na waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo. Pia, yalihudhuria na katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi; waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na; waziri wa ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kutoka mikoa ya Manyara, Morogoro na Dar es Salaam walihudhuria mazishi hayo yaliyotanguliwa na shughuli za kuaga mwili zilizofanyika nyumbani kwa marehemu eneo Majengo mjini Korogwe. Bendera alifariki dunia Desemba 6 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jafo, Mnyeti wamlilia Bendera

Akizungumza katika mazishi hayo, Jafo alisema Serikali imepokea kwa majonzi msiba huo na hasa ikizingatiwa Bendera alifanya kazi kwa uadilifu akiwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kisha Manyara. Alisema Bendera ni miongoni mwa viongozi wachache waliokuwa na hekima na busara katika kutekeleza majukumu yake, hivyo kutumikia nyadhifa kadhaa ndani ya Serikali. “Viongozi kama Joel Bendera ni wa mfano hasa kutokana na uchapaji kazi wake, hivyo viongozi waliopo wanapaswa kuyaenzi mambo makubwa aliyokuwa akiyafanya wakati wa utumishi wake kwa lengo la kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo kwenye maeneo yao,” alisema.

“Nimefurahi kumuona Rais mstaafu Jakaya Kikwete hapa ambaye naye alifanya kazi naye kwa uadilifu mkubwa.”

Mbali ya ukuu wa mkoa, Bendera aliwahi kuwa mbunge wa Korogwe Mjini na naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala wa Rais Kikwete.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema Bendera alimkabidhi ofisi Oktoba 31 baada ya kustaafu Oktoba 26, na alimuusia mambo 10 yakiwamo upendo, uaminifu, subira, uvumilivu, ucha Mungu, upatanishi, kupenda haki, ukweli, amani na uzalendo.

“Aliniambia kwamba haya mambo 10 Mnyeti yatakuvusha na akaongeza kuwa uzalendo wake uko ndani ya damu, uwajibikaji wake upo asilimia 100, kufanya kazi miaka 45 serikalini bila kashfa si jambo dogo ni uadilifu,” alisema Mnyeti.

Mamia wamuaga Joyce Dar

Mamia ya waombolezaji walijitokeza jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuaga mwili wa aliyewahi kuwa mwandishi mwandamizi wa habari za siasa wa gazeti la Mwananchi, Joyce Mmasi.

Joyce anayetarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Mbokomu wilayani Moshi alifariki dunia Desemba 6 katika Hospitali ya TMJ baada ya kuugua saratani ya damu.

Shughuli za kuaga mwili wake awali zilifanyika nyumbani kwake Mbezi Kibanda cha Mkaa na baadaye Mnazi Mmoja ambako pia wanasiasa walijitokeza.

Ibada ya kuaga mwili iliongozwa na mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luis, Richard Lucas ambaye alisema maisha aliyoishi Joyce yawe fundisho kwa waliobaki duniani.

Andrew Kamugisha ambaye ni mume wa Joyce alitoa shukrani kwa ndugu, jamaa na marafiki waliokusanyika katika msiba huo akiweka wazi namna alivyojengwa katika mambo mengi na mkewe.

“Mke wangu alikuwa mkurugenzi mwenzangu Shule ya Macmillan, kila tunachokifanya hakika tulifanya kwa pamoja. Nashukuru kwa kuwa tumekuwa pamoja kipindi cha kumuuguza mpaka anafariki na mpaka sasa tupo pamoja,” alisema akitoa shukrani wa waombolezaji.

Akizungumza katika shughuli hiyo, mhariri mtendaji mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji, Francis Nanai alisema Joyce alikuwa mwandishi wa habari lakini pia mjasiriamali.

Alisema MCL inaungana na familia na wanahabari kuomboleza kifo cha Joyce kwa kuwa ameacha mfumo katika baadhi ya vikundi alivyojiunga ikiwamo miradi iliyowezesha vikundi hivyo kujiinua.

“Hili ni fundisho kwetu kwamba tunahitaji kuishi maisha ya kujiongeza, maana Mmasi alikuwa mwanachama mzuri wa Saccos yetu ya Mwananchi na alitoa mawazo ambayo yamesaidia maendeleo ya Saccos na kampuni, japokuwa aliondoka kwenda kusoma lakini aliendelea kushiriki Saccos na hata Vicoba, tunawapa pole familia,” alisema Machumu.

Katibu tawala wa Halmashauri ya Kigamboni, Rahel Mhando alitoa pole akisema: “Jambo zuri ambalo tumeliona siku za hivi karibuni ni ushirikiano baina ya wana tasnia na namna gani unatuunganisha na kukuza taaluma hii ya habari nchini.” Mhando kitaaluma ni mwandishi wa habari. Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Susan Lyimo alisema yeye ni mwakilishi wa dada wa Joyce kwa kuwa alimfahamu tangu akiwa tumboni mwa mama yake kwa kuwa wanatoka kijiji kimoja.

“Tumezoeana akiwa binti mkubwa, amekulia kwenye tasnia nilimjua kwa tabia zake, natoa pole nyingi kwa Taifa tumepoteza mwanahabari makini sana, amefariki akiwa na miaka 42 bado mdogo sana anatufanya tuyatafakari maisha yetu,” alisema Susan. Imeandikiwa na Burhani Yakub, Jackline Masinde na Herieth Makwetta.