Joto la uchaguzi wa marudio lapanda

Mgombea Udiwani Kata ya Mwaka Kati kwa tiketi ya CCM, Ayub akionyesha dirisha la chumba chake anacholala akidai watu wasiojulikana walifanya jaribio la kuchoma nyumba yake usiku wa kuamkia juzi katika eneo hilo, wilayani Tunduma, mkoani Simiyu. Picha na Godfrey Kahango

Muktasari:

Kampeni za uchaguzi huo wa Agosti 12 utakaofanyika katika Jimbo la Buyungu na kata 77 zilianza jana, huku wagombea wa CCM wakipita bila kupingwa katika kata 12 lakini wapinzani wao wakilalamika kuchezewa rafu.

Dar/mikoani. Joto la uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani limepanda, matukio ya wagombea kupita bila kupingwa na malalamiko ya wengine kutotendewa haki yakitawala.

Kampeni za uchaguzi huo wa Agosti 12 utakaofanyika katika Jimbo la Buyungu na kata 77 zilianza jana, huku wagombea wa CCM wakipita bila kupingwa katika kata 12 lakini wapinzani wao wakilalamika kuchezewa rafu.

Vyama vya ACT- Wazalendo na Chadema vinalalamika wagombea wao kuenguliwa vikidai ni njia ovu ya kuiwezesha CCM kuibuka na ushindi.

Mbali ya hayo, baadhi ya viongozi wa Chadema jimboni Tunduma mkoani Songwe inadaiwa wamekimbilia mafichoni wakihofia kukamatwa, huku mbunge wa jimbo hilo (Chadema), Frank Mwakajoka aliyekuwa akishikiliwa rumande tangu juzi akiachiwa jana.

Hayo yakiendelea, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Dk Athuman Kihamia alisema jana kuwa leo atatoa taarifa ya kilichojiri wakati wa uchukuaji na urejeshaji fomu wagombea.

“Taarifa nzima ya kinachoendelea, zikiwamo kata walizopita wagombea bila kupigwa, malalamiko tutazitoa kesho (leo) kwani leo (jana) ni Jumapili,” alisema Dk Kihamia.

ACT, Chadema wanena

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema hadi juzi pazia la kurejesha fomu likifungwa, wagombea 15 wa udiwani wa chama hicho walirejesha fomu.

“Wagombea wanne wamefanyiwa vitimbi na kuenguliwa. Wagombea watatu kwenye kata zilizopo Tunduma hawakuteuliwa kwa kigezo kwamba si raia,” alisema Shaibu.

Alisema kuna pingamizi kwenye Kata ya Turwa wilayani Tarime, Mara ambalo walikuwa wakilishughulikia kuhakikisha wagombea wanateuliwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu.

Kwa Chadema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema alisema wanafuatilia katika maeneo yote kilichotokea na watatoa taarifa.

CCM yapeta kata 12

Jijini Arusha, CCM imepita katika kata saba kati ya 20 na kata tano za Tunduma mkoani Songwe baada ya wagombea wake kutokuwa na wapinzani.

Kata sita kati ya hizo, wagombea wa Chadema walishindwa kurejesha fomu na katika kata nyingine mgombea wa Chadema inaelezwa hajui kusoma.

Wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri za Longido, Monduli na Ngorongoro waliozungumza jana walisema baada ya wagombea hao kuondolewa, utaratibu wa uchaguzi katika kata nyingine unaendelea.

Kata hizo saba ni Alang’atadapash, Kamwanga, Soitsambu, Pinyinyi, Ngoile, Ngorongoro, Nararami na Loksale.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema chama hicho kina uzoefu na uchaguzi mdogo, hivyo kinafuatilia kwa makini uchaguzi kwenye kata zote huku Katibu wa Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe akisema wamejipanga kuibuka na ushindi katika kata zote 20.

Wagombea wa CCM katika kata 19 mkoani humo walikuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia chama tawala.

Huko Tunduma, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Castory Msigala jana jioni aliwakabidhi madiwani watano wa CCM barua za utambulisho kwamba wamepita bila kupingwa na sasa watapewa hati zao Agosti 12.

Waliokabidhiwa barua hizo ni Simon Mbukwa wa Kata ya Karoleni, Julius Mwavirenga (Sogea), Amos Nzunda (Mpemba), Frank Mponzi (Mjengo) na Ayub Mlimba (Mwaka Kati).

Chadema Serengeti

Hatua ya mgombea udiwani wa Ikoma wilayani Serengeti, Kenedy Josephat (Chadema) kushindwa kurejesha fomu ya uteuzi imemweka matatani katibu wa chama hicho wilayani humo, Julius Anthony akishutumiwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini anayetokana na Chadema alisema Anthony alishiriki kukihujumu chama hicho kwa kuandika vibaya barua za mgombea ili awekewe pingamizi.

“Mwaka 2015 katibu alishiriki kuwaandikia wagombea wote wa Chadema barua kwa usahihi na hapakuwa na pingamizi, kwa hili alifanya makusudi kwa kuwa huwezi kuandika barua haina tarehe, haina muhuri wala jina la aliyeandika halafu unampa mgombea,” alisema Porini.

Alisema fomu eneo la muhuri wa chama aligonga wa katibu; sehemu za muhuri aliweka saini; tarehe ya uteuzi ilikuwa Julai 14 yeye akaandika Julai 12. Pia, anatuhumiwa kuficha muhuri.

Anthony aliyewahi kuwa katibu wa tawi wa CCM alikiri kuandika barua kwa makosa hasa maeneo ya tarehe, akisema hayo yangeweza kurekebishwa.

Hata hivyo, akijitetea Anthony aliibua hoja nyingine akidai, “Kuna diwani wa Chadema wa Nyansurura, Francis Garatwa ndiye aliyekuwa anazunguka na mgombea na kumchelewesha, hayo mengine wanasaka sababu ya kukuza maneno,” alisema Anthony.

Garatwa alikanusha madai hayo akisema sababu za kukosa kuteuliwa kwa mgombea wao ni kiapo kutokana na katibu (Anthony) kudai hana muhuri ili augonge kwenye barua ya utambulisho.

Fomu zakataliwa

Wilayani Mbulu, Manyara, fomu za wagombea wawili wa Chadema wa kata za Tumati na Hayderer zilikataliwa ikielezwa zimekosewa kujazwa.

Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema fomu ya Zacharia Nihhi wa Tumati na Daniel Boa wa Hayderer ziliwekewa pingamizi baada ya kukosewa kujazwa.

“Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi, fomu za wagombea zimekosewa na wamewekewa pingamizi nasi tumewaandikia barua wajibu ndani ya saa 24 na baada ya siku saba Tume itatoa majibu,” alisema Kamoga.

Alisema fomu za wagombea wa CCM Justin Masuja (Hayderer) na Paulo Axweso (Tumati) hazina upungufu hivyo wamepitishwa kugombea.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Manyara, Gervas Sulle alisema fomu hizo zilijazwa kikamilifu kwa kuwa walifuata maelekezo.

Mgombea anusurika

Mgombea udiwani Kata ya Mwaka Kati (CCM), mkoani Songwe, Ayoub Mlimba amedai alinusurika kifo baada ya watu wasiojulikana kuchoma nyumba yake moto.

Alisema wakati mkewe akikimbilia vyumbani kuwaokoa watoto, alikwenda mlangoni kuomba msaada kwa majirani na katika harakati za kuuzima alianguka na kuungua miguu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa simu.

Mbunge aachiwa

Mwakajoka pamoja na Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Mkoa wa Songwe, Ayoub Sigakonamo waliokamatwa juzi, waliachiwa jana huku wanachama zaidi ya 15 wakiendelea kushikiliwa.

Boniface Mwambukusi ambaye ni wakili wa Mwakajoka akizungumza baada ya mteja wake kuachiwa, alisema walielezwa kwamba wanatuhumiwa kuchoma moto nyum-ba nyumba ya mgombea udiwani wa CCM Kata ya Mwaka Kati, Mlimba.

Juzi, akizungumzia kukamatwa kwa Mwakajoka, mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga alisema miongoni mwa waliokamatwa ni baadhi ya madiwani, wanachama wa Chadema na walinzi wa chama hicho maarufu kama red brigade.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alikataa kuzungumzia suala na mwandishi kwa si-mu akisema hawezi kuamini kama anayezungumza naye ni mwandishi wa habari.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola (Dar), Godfrey Kahango (Tunduma), Anthony Mayunga (Mara), Muhingo Mwemezi (Buyungu), Mussa Juma (Arusha) na Joseph Lyimo (Babati).