Jumuiya A. Mashariki kushusha gharama miamala kwenye ATM

Muktasari:

Mpango huo unaoihusisha Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda ulitarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2015 lakini ulisitishwa baada ya mawaziri wa fedha kutofikia muafaka.

Dar es Salaam. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kufanya marekebisho ya sheria za fedha ili kuruhusu kushusha gharama za miamala inayofanywa na wananchi wanaotembelea nchi nyingine.

Mpango huo unaoihusisha Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda ulitarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2015 lakini ulisitishwa baada ya mawaziri wa fedha kutofikia muafaka.

Hata hivyo, wiki iliyopita, wawakilishi wa mataifa hayo walikutana jijini Mombasa, Kenya kwenye mkutano ulioridhia kufanyika kwa utafiti utakaoruhusu wateja wa benki moja kutumia huduma za mashine ya kutolea fedha (ATM) za benki nyingine katika nchi jirani kwa gharama nafuu.

Habari iliyoripotiwa na gazeti la Business Daily imemnukuu ofisa mtendaji mkuu wa Jumuiya ya Benki za Kenya (KBA), Habil Olaka akisema mpango huo utaongeza matumizi ya huduma za fedha kwa wananchi wa mataifa hayo manne na kuongeza kiasi cha malipo kinachofanywa kwa miamala inayovuka mipaka ya nchi moja.

Mpango huo unatokana na mapendekezo yaliyotolewa na utafiti uliofanywa mwaka 2014 na kampuni ya Ernst&Young (Uganda) kwa ufadhili ya Dola 14 milioni za Marekani (zaidi ya Sh31.5 bilioni) kutoka Benki ya Dunia baada ya kupata baraka za magavana wa benki kuu za mataifa husika.

Licha ya magavana hao kuridhia kutekelezwa kwa mpango huo tangu Mei 2014 ili kufanikisha miamala kwa wakati kwa kutumia sarafu yoyote ya nchi wanachama, kikwazo kilikuwa sheria na sera zitakazofanikisha suala hilo.

Wateja wa benki ndani ya EAC wanatozwa Dola 2.5 (Sh5,625) kila wanapotumia ATM iliyopo nje ya mipaka ya nchi zao lakini utakapoanza kutekelezwa mpango huo, gharama hizo zitapungua mpaka Dola 0.8 (Sh1,800) kwa kila muamala.

Licha ya gharama za kila muamala utakokuwa unafanywa kwenye ATM, benki kuu ya kila nchi itakuwa na jukumu la kupanga kiwango cha kubadilishia fedha hivyo kuepuka hasara ambayo angeweza kuipata mteja anapokwenda nchi jirani.

Kutokana na mpango huo, kwa mfano, mtajea wa Benki ya NMB anayetumia kadi ya kutolea fedha anayeenda nchini Kenya ataweza kutumia ATM za Benki ya Equity kwa gharama ya Sh1,600 kwa kila muamala huku akibadilisha fedha zake kwa kutumia viwango vilivyowekwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK).