Magufuli kufungua mkutano Jumuiya ya Wazazi

Muktasari:

Mkutano huo utatathmini utendaji wa Jumuiya ya Wazazi kwa miaka mitano iliyopita na ijayo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa Taifa wa tisa wa Jumuiya ya Wazazi mjini Dodoma.

Mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete pia umehudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Mama Maria Nyerere; na viongozi wengine wa CCM.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo atakabidhi mikoba kwa kiongozi mpya atakayechaguliwa.

Imeelezwa mkutano huo utakuwa na mambo mawili; moja ni kutathmini utendaji wa jumuiya hiyo kwa miaka mitano iliyopita na ijayo na pili; uchaguzi wa viongozi wakiwamo mwenyekiti, makamu wake na wajumbe.

Uchaguzi ndani CCM na jumuiya zake ni sehemu ya utekelezaji wa kalenda ya chama hicho kwa mwaka 2017. Umefanyika kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.