KCB kuendelea kupunguza riba

Muktasari:

Kauli ya benki hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kuwaomba washushe zaidi riba. Kwa sasa riba ni asilimia 15


Dar es Salaam. Benki ya KCB Tanzania imesema itaendelea kupunguza riba ya mikopo ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi kunufaika nayo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Julai 9, 2018 na  mkurugenzi mkuu wa KCB Tanzania, Cosmas Kimario kwenye uzinduzi wa tawi la benki hiyo  Mbagala Zakhem jijini hapa baada ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kuwaomba wapunguze riba zao.

"Kwa sasa riba yetu ni asilimia 15, tumeipunguza kutoka asilimia 20 iliyokuwepo awali lakini bado tunaendelea kuangalia namna ya kuishusha zaidi kulingana na kiasi cha fedha anachochukua mkopaji na muda atakaotumia kulipa," amesema Cosmas.

Amesema kwa wanaokopa kwa sarafu ya Dola ya Marekani riba yao ni asilimia nane tu.

Mbali na kupunguza riba, Cosmas amesema benki hiyo ipo katika mkakati wa kusogeza huduma karibu na wateja wake katika maeneo tofauti ili kupunguza muda wa kutafuta huduma. 

Kwa upande wake Dk Ashatu ameitaka benki hiyo kuangalia namna ya kuifikia sekta isiyo rasmi hususan kilimo ili kuongeza uzalishaji wa malighafi zitakazokidhi mahitaji ya viwanda.

"Hakuna viwanda bila kilimo, wasipokuwapo wakulima hatuwezi kuwa na viwanda tunavyovihitaji. Wafikieni wakulima kwa sababu katika eneo hili bado hatujafanya vyema," alisema Dk Kijaji.

Endapo mkulima atawezeshwa kwa mikopo, amesema itawezesha kukuza uchumi na Tanzania kuwa na kipato cha kati kabla ya mwaka 2025.

Amesema mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kusini imeonyesha mwamko na wameweza kuongeza uzalishaji wa mazao yao kwa kiasi kikubwa.

"Tunategemea kuona riba mnazowatoza Watanzania zinakuwa za chini kwa sababu hatuna haja ya kuwaumiza kwa riba kubwa," amesema.