KCBL yakopesha wakulima Sh28 bil

Muktasari:

  • Benki hiyo inayomilikiwa na wazalendo kwa asilimia 100, ilifunguliwa mwaka 1996 na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ikiwa ya kwanza ya ushirika kufunguliwa nchini.
  • Meneja Mkuu wa KCBL, Joseph Kingazi alisema mikopo hiyo ilitolewa kwa wakulima wa zao la kahawa.

Moshi. Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), imetoa mikopo ya Sh28 bilioni kwa wakulima wa kahawa tangu mfumo wa stakabadhi ghalani uanzishwe na benki hiyo mwaka 2002.

Benki hiyo inayomilikiwa na wazalendo kwa asilimia 100, ilifunguliwa mwaka 1996 na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ikiwa ya kwanza ya ushirika kufunguliwa nchini.

Meneja Mkuu wa KCBL, Joseph Kingazi alisema mikopo hiyo ilitolewa kwa wakulima wa zao la kahawa.

“KCBL imekuwa mwanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ghalani. Kwa sasa huu mfumo umeweza kuenea na kutumika sehemu mbalimbali hasa kwenye mazao ya pamba na korosho,” alisema.

Benki hiyo ina wana hisa 245 ambao ni Vyama vya Ushirika vya Mazao (Amcos) na vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) pamoja na watu binafsi.

Kingazi alisema KCBL inajipanga kuongeza ukopeshaji katika sekta mbalimbali kama za kilimo, biashara ndogondogo, utalii na kwenye sekta ya ujenzi.

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro (Kncu), Honest Temba alisema benki hiyo ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wakulima.

“Unajua si benki nyingi zinakopesha wakulima, lakini KCBL ndiyo imekuwa mstari wa mbele kukopesha wakulima wa kahawa na ni mhimili mkubwa katika maendeleo ya sekta hii,” alisema.