KCU yatoa onyo ikitishia kutaifisha kahawa ya wakulima

Muktasari:

KCU imeonya kuwa wakulima watakaofanya hivyo watakabiliana na adhabu ya kutaifishwa kwa mazao yao.

Siku chache baada ya wabunge wa Kanda ya Ziwa kucharuka bungeni kuhusu mfumo mpya wa uuzaji wa kahawa, Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU), kimeibuka na kutoa onyo kwa wakulima watakaouza zao hilo nje ya mfumo.

KCU imeonya kuwa wakulima watakaofanya hivyo watakabiliana na adhabu ya kutaifishwa kwa mazao yao.

Akizungumza jana, mwenyekiti wa Bodi ya KCU, Onesmo Niyegila alisema kuwa utaratibu wa sasa ni kwa kahawa yote kukusanywa kupitia kwenye vyama vya ushirika na kupelekwa sokoni mjini Moshi ambapo wanunuzi wote watanunulia hapo mnadani.

“Kwa mantiki hiyo hakuna mkulima yeyote atakayeruhusiwa kuuza kahawa nje ya mfumo wa ushirika,”alisema.

Kuhusu bei ya kahawa, Niyegila alisema malipo ya awali yaliyopendekezwa na menejimenti na bodi ya chama hicho katika mkutano mkuu uliofanyika Machi 27 ni Sh 1,000 kwa kilo ya kahawa ya maganda. Hata hivyo, baada ya mjadala wanachama waliagiza kupitiwa upya kwa makisio hasa kwa upande wa malipo ya awali na kuangalia namna ya kupandisha kiwango cha malipo ya wali. “Kiwango kipya pendekezwa kitawasilishwa kwa mrajisi wa vyama vya ushirika kwa ajili ya kuidhinishwa,”alisema.

Kaimu mrajisi wa vyama hivyo nchini, Tito Haule alisema mfumo huo una faida nyingi ikiwamo kuongeza bei ya soko. “Kwa mfano katika korosho bei ya korosho imeongezeka kutoka Sh800 hadi Sh4,125 baada ya kuanza utekelezaji wa mfumo huu,”alisema.

Akichangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2018/19, mbunge wa Nkenge (CCM), Dk Diodorus Kamala alisema utaratibu uliofanyika kuuza kahawa katika vyama vya ushirika ni mzuri, lakini unahitaji maandalizi kabla ya kuuanza.