KESI MAUAJI YA BILIONEA MSSUYA-Ushahidi wa DNA waibua mjadala mahakamani

Watuhumiwa wa Kesi ya mauwaji ya mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya wakipelekwa kwenye chumba cha Mahakama Kuu kanda ya Moshi, mkoani Kilimanjaro jana. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

Sampuli za damu na mate zilizochukuliwa kwa mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa na wa sita, Sadik Jabir, zilioana na sampuli zilizochukuliwa katika jaketi lililopatikana eneo la tukio.

Mahakama imepokea kama kielelezo, ripoti ya uchunguzi wa (DNA) za washtakiwa wawili katika kesi ya mauaji ya makusudi ya mfanyabiashara tajiri wa Mererani, Erasto Msuya.

Sampuli za damu na mate zilizochukuliwa kwa mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa na wa sita, Sadik Jabir, zilioana na sampuli zilizochukuliwa katika jaketi lililopatikana eneo la tukio.

Jaketi hilo ndilo ambalo mashahidi waliotangulia wanadai liliachwa na washtakiwa wawili wa mauaji hayo katika kijiji cha Orkolili wilayani Siha wakati wakitoroka baada ya pikipiki yao kupata pancha.

Katika ushahidi wake alioutoa mwaka 2015, shahidi wa tatu, Raphael Karoli, alidai koti hilo lilitelekezwa na watu wawili baada ya pikipiki kupata pancha na walipowafuata walifyatua risasi.

Jaketi hilo, kofia ngumu na pikipiki aina ya Toyo, ndivyo ambavyo mashahidi wa upande wa mashtaka wanadai vilitelekezwa na watu hao waliokuwa na silaha siku ya mauaji Agosti 7, 2013.

Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Jaji Salma Maghimbi, shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka, Gloria Omary alidai sampuli zilizochukuliwa kwenye jaketi zilioana na sampuli za washtakiwa.

Shahidi huyo ambaye mwaka 2013 alikuwa mtaalamu katika Idara ya Sayansi Jinai na DNA katika ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali, alieleza sampuli hizo alizipokea ofisini kwake jijini Dar es Salaam Oktoba 3, 2013.

Kulingana na shahidi huyo, siku hiyo alipokea kifurushi kilichofungwa kwa lakiri kutoka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Arusha, ambao nao walikipokea kutoka ofisi ya RCO mkoani Kilimanjaro.

Alidai kifurushi hicho kilikuwa na vipande vya nguo aina ya jaketi na sampuli za damu na mate za washtakiwa hao wawili na kwamba, alitakiwa kufanya uchunguzi wa chembechembe za asili za urithi.

Shahidi huyo ambaye kwa sasa anafanya kazi maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), alidai vielelezo hivyo vilikuwa vikihusiana na jalada la mauaji ya bilionea Erasto Msuya.

Pamoja na kupokea sampuli za vipande vya jaketi vya maeneo ya mfuko, mkono na shingo pia alipokea jaketi ambalo sampuli hizo zilichukuliwa na sampuli za mate na damu za washtakiwa.

Alieleza katika uchunguzi huo, baadhi ya sampuli hazikutoa majibu na baadhi ya sampuli zilionyesha matokeo kuwa DNA za washtakiwa, zilioana na sampuli zilizochukuliwa katika jaketi hilo.

Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula kutoa ushahidi wake, shahidi huyo aliomba mahakama ipokee ripoti ya uchunguzi aliyoiandaa yeye mwenyewe kama kielelezo.

Jopo la mawakili wa utetezi linaloundwa na mawakili Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na John Lundu, haukuwa na kipingamizi na ripoti hiyo ikapokelewa kama kielelezo P17. Hata hivyo, kulitokea mvutano wa kisheria wakati shahidi huyo alipotaka kulitoa jaketi hilo kwa ajili ya utambuzi tu (Identification purposes), mawakili wa utetezi walipinga.

Akiwasilisha hoja za kupinga kupokewa kwa jaketi hilo, wakili Magafu alidai ili kitu chochote kipokewe kwa ajili ya utambuzi, lazima kiwe na sifa ya kupokewa kama kielelezo.

Magafu alidai katika ushahidi wake, shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Raphael Karoli alieleza yeye ndiye aliyeokota jaketi la rangi ya kaki lililoachwa na washtakiwa akalikabidhi polisi.

“Prosecution (upande wa mashtaka) haukumtaka huyu shahidi wao kuli tender (kulitoa) hilo jaketi kama kielelezo. Shahidi wa tisa (Samwel Maimu) aliyekabidhiwa hakulitoa kama kielelezo,” alidai Magafu na kuongeza:

“Leo hii tunaletewa jaketi lililokatwakatwa vipande na hatujaelezwa vilichukuliwa na nani vikawekwa kwenye bahasha hadi vikamfikia PW25 (shahidi wa 25) aliyeko hapo kizimbani.

“PW3 (shahidi wa tatu) alilitambua jaketi wakati anatoa ushahidi wake mwaka 2015 na jaketi hilo lilikuwa halijakatwakatwa vipande. Leo hii tunaletewa jaketi limeshakatwakatwa.”

Alidai kwa ushahidi wake mwenyewe alioutoa jana, shahidi wa 25 (Gloria) ameieleza mahakama kuwa jaketi hilo lilipelekwa kwake Oktoba 2, 2013 likiwa limeshakatwakatwa.

“Imekuaje PW3 (shahidi wa tatu) alilitambua jaketi hilo mwaka 2015 halijakatwa vipande vipande, lakini hili linalotaka kupokewa leo (jana) kwa utambuzi limekatwakatwa?” Alihoji.

Magafu alidai shahidi huyo anakosa sifa ya kulitoa jaketi hilo kwa utambuzi kwa sababu hajaeleza upatikanaji wake kutoka eneo la tukio, hadi maabara Arusha na baadaye kumfikia yeye.

“Kwa mujibu wa ushahidi wa PW3 inaonekana tumeletewa kitu kingine kabisa leo,” alidai Magafu, kauli ambayo ilimnyanyua wakili wa Serikali mkuu, Peter Maugo, akipinga hoja hiyo.

Maugo alidai anachokifanya msomi mwenzake ni kufanya mlinganisho wa ushahidi wa mashahidi, jambo alilodai kwa hatua waliopo si sahihi bali ilipaswa ifanywe wakati wa majumuisho ya kesi.

Hata hivyo, Magafu alidai wanachobishania ni uhalali wa kielelezo kinachoombewa kipokewe na mahakama kwa utambuzi kwa vile kinatofautiana na kilichotambuliwa na PW3.

“Tarehe 6/10/2015 tuliletewa koti zima wakati shahidi wa tatu anatoa ushahidi wake. Leo tunaletewa koti lililokatwakatwa. Hii ndiyo hoja yetu,” alisisitiza Magafu na Jaji akamruhusu alizungumzie.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavula alidai hoja za mawakili wa utetezi zimewahishwa (premature) kwa vile upande wa mashtaka haujafunga kesi yake. “Prosecution (upande wa mashtaka) hatujafunga kesi na huyu shahidi sio wa mwisho, hivyo kuiaminisha mahakama kwa kuegemea ushahidi wa PW3 na PW9 si sahihi,” alieleza Chavula na kuongeza:

“Wenzetu wanasema shahidi wa tatu alipolitambua jaketi lilikuwa halijakatwa na kinacholetwa leo (jana) ni tofauti, sisi tunasema si sahihi wala kumbukumbu ya hicho kitu haipo.”

Alidai siku alipotoa ushahidi wake, shahidi wa tatu alieleza tu ataweza kulitambua jaketi hilo kwa rangi yake na hakuna kumbukumbu za mahakama kuwa alilikagua.

“Hata wakati analitambua (shahidi wa tatu) hapa mahakamani, hakulikagua huko ndani. Alionyeshwa jaketi kwa nje kwa ujumla wake akasema analitambua kwa rangi ya kaki.

“Hoja zinazoibuka leo kuwa sio lile, hazina mashiko wala mantiki. Kesi inaendelea na tuna mashahidi 50 na huyu leo ni wa 25 nani kasema hatakuja shahidi mwingine kulikabidhi?” Alihoji.

Akitoa uamuzi wake mdogo, Jaji Maghimbi alikubaliana na hoja za mawakili wa Serikali na kueleza kuwa anachokitolea ushahidi ni kile alicholetewa kukifanyia kazi.

“Alichokisema shahidi ni kwamba alichokipata kutoka maabara ya Arusha ni mfuko ambao ndani yake kulikuwa na sampuli. Tunawezaje kutenganisha jaketi na sampuli alizozipokea pamoja?” Alihoji Jaji.

Jaji Maghimbi alilikataa pingamizi la mawakili wa utetezi na kukubali jaketi hilo lipokelewe kwa utambuzi, hivyo wakili Magafu akapata fursa ya kumhoji shahidi kuhusiana na ushahidi wake.

Alipoulizwa aliyemtajia majina yanayoonekana katika sampuli alizozipokea, shahidi huyo alidai majina hayo yalikuwapo katika nyaraka za utambuzi zilizowasilishwa kwake na RCO.

Magafu alimuuliza shahidi huyo kama anafahamu sampuli za damu na mate za washtakiwa hao eneo (place) zilikochukuliwa, alisema yeye hafahamu.

Kuhusu kama aliwahi kuletewa washtakiwa hao ili achukue upya sampuli za damu na mate, shahidi huyo alisisitiza kuwa sampuli alizoletewa alipelekewa na ofisi ya RCO Kilimanjaro.

Magafu alimuuliza shahidi huyo kuwa anazungumziaje kauli ya wateja wake (washtakiwa) wanaosema hawakuwahi kuchukuliwa mate wala damu, yeye alisema hajui.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Mussa.